China yampa nishani ya juu Dk. Salim

0
537

MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

RAIS wa Jamhuri ya Watu wa China, Xi Jinping,  amemtunukia Waziri Mkuu Mstaafu, Dk. Salim Ahmed Salim, nishani ya juu ya urafiki ya Jamhuri ya Watu wa China ikiwa ni sehemu ya matukio ya maadhimisho ya miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China.

Jinping alimtunuku rasmi tuzo hiyo inayomfanya Dk. Salim kuwa mwafrika wa kwanza kupewa heshima na tuzo hiyo ya juu katika historia ya China, katika maadhimisho rasmi yaliyofanyika jana asubuhi, Septemba 29 jijini Beijing.

Nishani hiyo ilipokelewa na binti wa Dk Salim, Maryam ambaye pia ni Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini Albania kwa niaba ya baba yake kutokana na kushindwa kuhudhuria kwa sababu za kiafya  ambapo katika tukio hilo, Serikali ya Tanzania iliwakilisha na Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki.

Hafla hiyo kubwa ya kitaifa ya kukabidhi nishani ilihudhuriwa na viongozi waandamizi wa Chama na Serikali ya China akiwemo Makamu wa Rais Wang Qishan, Waziri Mkuu Li Keqiang, Spika wa Bunge Li Zhanshu na  ambao wote ni wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China na Baraza la Taifa. 

Mbali na Dk.Salim,  wengine waliotunukiwa Nishani ya Urafiki ni pamoja na Kiongozi wa Chama cha Kikoministi cha Cuba,  Jenerali Raul Castro, Dada wa Mfalme wa Thailand Maha Chakri Sirindhorn, Kiongozi wa Jumuiya ya Urafiki ya China na Urusi , Galina Kulikova, Waziri Mkuu Mstaafu wa Ufaransa Jean-Pierre Raffarin na Isabel Crook  kutoka Canada. 

Vilevile Rais Xi alitoa nishani ya Jamhuri na nishani ya heshima ya taifa kwa raia 36 wa China kwa kutambua mchango wao mkubwa katika maendeleo ya Taifa la China kupitia kazi zao katika fani mbalimbali.

Nishani ya juu ya urafiki ya taifa la China imetolewa kwa Dk. Salim, kutokana na mchango wake wa kuiwezesha Jamhuri ya Watu wa China kuwa Mwanachama wa Umoja wa Mataifa mwaka 1971 alipokuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa (UN). 

Aidha, mchango wa Dk. Salim katika kuimarisha uhusiano kati ya China na Tanzania wakati aliposhikilia nyadhifa mbalimbali umetajwa kama sababu ya kutunukiwa nishani hiyo.

Pia inaelezwa kuwa mchango wa Dk.Salim katika kujenga uhusiano kati ya China na Afrika akiwa na nafasi ya Katibu Mkuu wa OAU umetajwa kuwa sababu nyingine ya kutunukiwa Nishani.

Tukio la kutoa nishani lilitangazwa moja kwa moja kupitia Televisheni zote za Jamhuri ya Watu wa China na kushuhudiwa na watu zaidi ya milioni 500.

Kwa mujibu wa maelezo ya Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki , alisema tukio hilo limeshuhudiwa na mamilioni ya wachina hususan vijana walipata fursa ya kufahamu nafasi na mchango wa Tanzania na Bara la Afrika katika historia ya taifa lao.

Aidha Balozi Kairuki alieleza kwamba maadhimisho ya miaka 70 ya Jamhuri ya Watu wa China mwaka huu yanaambatana na maadhimisho ya miaka 55 ya urafiki na udugu kati ya China na Tanzania kufuatia kuanzishwa kwa mahusiano rasmi ya kidiplomasia mwaka 1964.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, alisema tuzo hiyo ni heshima kwa taifa.

Profesa Kabudi alisema Watanzania wanatakiwa kuyafanya majukumu ya kitaifa wanayopewa na viongozi wa serikali kwa uzalendo usiotiliwa mashaka, uaminifu na ufanisi kama walivyoelekezwa wakati wa kukabidhiwa majukumu hayo kwa faida ya nchi.

“Dk. Salim Ahmed Salim ni mtumishi mwaminifu na mzalendo kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ameitumikia nchi katika nafasi mbalimbali kuanzia na ukurugenzi katika wizara ya Mambo ya Nje na Ushrikiano wa Afrika Mashariki balozi katika nchi za Misri, India,China na Umoja wa Mataifa ,” alisema

Kwa upande wake mwanahabari mkongwe na mchambuzi wa masuala ua kiasiasa,  Jenerali Ulimwengu alisema tuzo hiyo inaonesha michango bora ya Dk. Salim Ahmed Salim na heshima kati ya China na dunia wakati alipokuwa akihudumu kama Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwa UN.

“Inastahili kutambuliwa mmoja wa wanadiplomasia mashuhuri wa Tanzania. Alikuwa na jukumu la kushikilia sababu ya China haswa katika kuandikishwa kwake UN mnamo 1971.

“Halafu, akiwa na umri wa miaka 28 tu, Dk. Salim alishambulia kampeni ili China ikubalike kwenye mkutano wa mataifa,” alisema Ulimwengu katika mahojiano yake na gazeti la China Daily.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here