Mwandishi wetu
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na lugha moja ya alama ili kuwezesha mawasiliano ya watumiaji wa lugha hiyo, na kwamba itaendelea kusimamia uendelezaji, usanifu na urasimishaji wa lugha ya alama nchini.
Amesema hatua hiyo itawezesha utoaji wa elimu katika ngazi mbalimbali pamoja na kuboresha mawasiliano katika jamii na tayari imetoa mafunzo ya lugha hiyo awamu ya kwanza kwa walimu 82 wa shule za Sekondari nchini na kwamba zoezi hilo ni endelevu.
Ameyasema hayo leo Jumamosi Septemba 28, wakati akihutubia wananchi kwenye kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Viziwi Duniani katika Uwanja wa Kichangani Kihesa, wilayani Iringa akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani humo.
“Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imeanza kurasimisha lugha ya Tanzania, kutayarisha vifaa vya kufundishia Lugha ya Alama ya Tanzania na kufundisha walimu katika shule za msingi na sekondari nchini, mchakato huo utachukua muda wa takribani miaka miwili kukamilika,” amesema.
Ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli imedhamiria na inatekeleza kwa dhati jitihada za kutoa kipaumbele kwa Watanzania wanyonge ambao hawakuwa wakinufaika ipasavyo na rasilimali za nchi.
“Serikali yenu sikivu inatambua vikwazo vya aina hiyo na inatekeleza maelekezo ya Ilani ya CCM ya 2015/2020, ambayo inaielekeza Serikali ihakikishe watu wenye ulemavu wanapata elimu kwa kupata vifaa maalumu na kushiriki katika shughuli za kijamii,” amesema Majaliwa.