27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Siku 14 za furaha, maumivu

GRACE SHITUNDU- DAR ES SALAAM

MAAMUZI na kauli zilizotolewa na baadhi ya viongozi nchini wakiongozwa na Rais Dk. John Magufuli ndani ya wiki mbili, zimeifanya nchi kuwa katika hali ya mchakamchaka ulioibua hisia tofauti za kifikra kwa jamii na wakati huo huo furaha, huzuni na kihoro miongoni mwa watendaji.

Uamuzi wa kupangua, kuteua baadhi ya watendaji, lakini pia kauli za kuonya na matumaini  zilizokuja baadaye, hasa kwa upande wa watuhumiwa ambao wanakabiliwa na kesi za uhujumu uchumi na utakatishaji fedha, ndio uliotoa taswira ya kuwapo kwa hali hiyo.

Septemba 22, mwaka huu, Rais Magufuli baada ya kuwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua, alitoa ushauri kwa Mkurugenzi wa Mashataka (DPP), Biswalo Mganga, kuwapa nafasi ya kuwasikiliza ndani ya siku saba, watuhumiwa wa uhujumu uchumi na utakatishaji wa fedha ambao wapo tayari kuomba msamaha na kurudisha fedha.

Wakati kikomo muda uliotolewa kikifikia jana, DPP Mganga amekiri maombi mengi kuwasilishwa kutoka pande mbalimbali nchini.

Miongoni mwa maombi yaliyowasilishwa na ambayo yalibainishwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam ni yale yanayomgusa Wakili maarufu nchini, Dk. Ringo Tenga na wakurugenzi wenzake wa Kampuni ya Six Telecoms.

Kesi za hujumu uchumi na zile za utakatishaji fedha ambazo hazina dhamana, zimesababisha watu wengi wakiwamo vigogo kadhaa kukaa magereza kama mahabusu kwa muda mrefu pasipo kujua hatma yao.

UTEUZI ULIOTIKISA

Kabla ya uamuzi huo dhidi ya watuhumiwa wa uhujumu uchumi na utakatishaji fedha, uamuzi wa mwanzo alioufanya ndani ya siku 14 wa kutengua nafasi za baadhi ya watendaji wake, kupangua na kuteua wengine wapya, nao ulionekana kuleta upepo mwingine.

Nafasi hizo ni mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya, manaibu katibu wakuu wa wizara na mabalozi katika vituo 11.

Walioachwa na maumivu katika uamuzi huo ni aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Steven Kebwe ambaye alitumbuliwa na nafasi yake kuchukuliwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Loata Sanare.

Aidha uteuzi ambao ulionekana kutikisa ni ule wa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Dk. Modestus Kipilimba aliyeteuliwa kuwa balozi baada ya hivi karibuni kumwondoa katika nafasi hiyo.

Taswira hiyo ndiyo iliyoonekana pia kwenye uteuzi wa Alphayo Kidata, aliyeteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara.

Kidata aliwahi kuwa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kabla uteuzi wake kutenguliwa na baadaye kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu Ikulu.

Baadaye Rais Magufuli alimteua  kuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada kabla ya kutengua uteuzi wake na kumrejesha nchini.

Rais Magufuli wakati akiwaapisha viongozi aliowateua, alisema sababu za kutumbua Dk. Kebwe ni kuwa alishindwa kushughulikia changamoto nyingi katika halmashauri zake huku migogoro ya ardhi ikiwa haiishi.

Kabla ya Dk. Kebwe kutumbuliwa, Rais Magufuli alikuwa amefanya uamuzi kama huo kwa Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Majura Kasika na aliyekuwa Mkurugenzi wake,  Mussa Mnyeti ikiwa ni baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kukerwa na migogoro yao ya mara kwa mara alipokuwa ziarani mkoani humo.

MAKONDA ROHO JUU

Pia wiki hizi mbili zimekuwa ni siku za wasiwasi kwa baadhi ya viongozi, hasa wa Mkoa wa Dar es Salaam baada ya Rais kuwanyooshea kidole mara mbili.

Awali ilikuwa ni Septemba 16 mwaka huu, Rais Magufuli alipofanya ziara ya kushtukiza  machinjio ya Vingunguti akiwa anatoka kuzindua kiwanda cha kutengeneza mabomba ya plastiki cha Pipe Industrial Co. Ltd. Kabla ya matukio hayo alizindua rada Uwanja wa Ndege wa Kimataifa  wa Julius Nyerere.

Akiwa katika machinjio ya Vingunguti, Rais Magufuli alionyesha kutoridhishwa na maendeleo ya mradi huo sambamba na ule wa Coco Beach na kumnyooshea kidole Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Pia Rais aliuagiza uongozi wa Halmashauri ya Ilala kutochangisha fedha katika machinjio ya Vingunguti hadi pale watakapokamilisha ujenzi wa machinjio ya kisasa jambo ambalo lilionekana kufurahiwa na wafanyabiashara katika machinjio hayo.

Hali hiyo ilionekana kuwaamsha watendaji wa Mkoa wa Dar es Salaam na siku mbili baadaye, Makonda aliunda kamati maalumu kusimamia utekelezaji wa miradi ya kimkakati katika mkoa huo ambayo itahusisha wataalamu mbalimbali wakiwemo maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Aidha, Mkoa wa Dar es Salaam ulinyooshewa tena kidole na Rais kuhusu mradi wa Coco Beach ambao alisema una maswali mengi.

Kwamba mradi huo kwanza unakinzana na sheria ya mazingira, unaingiliana na mradi wa ujenzi wa barabara ya daraja la Salender na kuwashangaa viongozi hao kuwahamisha wananchi pasipo kuwatafutia sehemu mbadala ya kufanya biashara zao.

Hali hiyo ilimfanya Makonda kukutana na viongozi na watendaji wake wa mkoa huku akidai kuwa anahujumiwa katika utendaji na kuahidi kuanza kufuatilia kila hatua ya miradi hadi nukta ya mwisho.

SIRRO NA KAULI MPYA

Wakati hayo yakijiri, kauli iliyotolewa wiki hii na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro, nayo imejenga hisia ya kubeba dhana ambayo imelenga kubadili mwelekeo wa awali wa utendaji wa Jeshi la Polisi.

Katika ufunguzi wa kikao kazi cha maofisa waandamizi wa polisi, kilichofanyika mapema wiki hii Dar es Salaam, Sirro aliainisha mambo kadhaa ambayo alisema yanalisumbua Jeshi la Polisi.

Mambo hayo ni unafiki, kutozingatia sheria, polisi kutokuwa makini wakati wanapopambana na wale wanaoleta fujo.

Kwa maneno yake mwenyewe, Sirro aliwanyooshea kidole wale wanaotolea macho wadhifa wake.

Sirro ambaye aliteuliwa Mei 28, mwaka juzi akichukua nafasi ya Ernest Mangu, alisema anatamani kumaliza kutumikia nafasi hiyo huku akiliacha Jeshi la Polisi likiwa na heshima yake.

Aidha, aliwataka polisi nchini kuongeza umakini katika utendaji wao wa kazi kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa huku akikumbusha vifo vya mwanafunzi Akwilina Akwiline na mwanahabari Daudi Mwangosi ambavyo alisema huwezi kuvipuuza.

Akwilina ambaye alikuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), aliuawa Februari 26, mwaka jana katika vurugu zilizohusisha polisi waliokuwa wakipambana na wafuasi wa Chadema waliokuwa wakielekea ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni kudai barua za mawakala wa kusimamia uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Kinondoni, Dar es Salaam.

Mwangosi aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Channel Ten, aliuawa Septemba 2, 2012 Kijiji cha Nyororo, Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa wakati akikusanya habari za ufunguzi wa tawi la Chadema.

Sirro alikiri kilichotokea Kinondoni na kusababisha kifo cha Akwilina kuna mahali Jeshi la Polisi halikutimiza wajibu wake sawasawa.

Kauli hizi za sasa za Sirro, baadhi wanaona zinaonekana kujitenganisha na kauli nyingine zilizopata kutolewa huko nyuma kuhusu matukio hayo na mengine ambayo yalilifanya Jeshi la Polisi linyooshewe vidole sana na jamii na kuvikwa taswira tofauti.

Kutokana na kauli hizo, lakini pia maamuzi yaliyofanywa ndani ya kipindi cha wiki mbili, vimeibua mitazamo tofauti kwa wananchi mbalimbali ambao baadhi wanaona kama kumechochewa na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa baadaye mwaka huu na Uchaguzi Mkuu mwakani.

Lakini pia wapo wanaoona kwamba Serikali imedhamiria kujisahihisha kwa upande mmoja na kwa upande mwingine kuendelea na msimamo wake wa kusimamia nidhamu kwa watendaji wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles