32.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 22, 2024

Contact us: [email protected]

Watuhumiwa ugaidi Arusha: Askari zaidi ya 100 wamwagwa mahakamani

Baadhi ya watuhumiwa wa kesi za kujishhughulisha na vitendo vya kigaidi wakishhushwa kwenye magari tayari kwa kusomewa mashitaka yao. Watuhumiwa hao 19 walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.
Baadhi ya watuhumiwa wa kesi za kujishhughulisha na vitendo vya kigaidi wakishhushwa kwenye magari tayari kwa kusomewa mashitaka yao. Watuhumiwa hao 19 walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.

ELIYA MBONEA NA JANETH MUSHI, ARUSHA

ULINZI mkali jana uliimarishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, wakati watuhumiwa wa vitendo vya ulipuaji mabomu jijini hapa walipofikishwa mahakamani.

Askari wasiopungua 100 wakiwamo wenye mbwa, askari wa usalama wa taifa, magereza, askari kanzu na askari polisi wenye bunduki na mabomu ya machozi walitanda eneo la mahakama na hivyo kuvuta hisia za wananchi wengi.

Hatua hiyo inaelezwa kuwa ililenga kuimarisha usalama wakati wa kesi ya watuhumiwa hao 19 wanaokabiliwa na mashtaka ya kujihusisha na vitendo vya ugaidi kwa kulipua mabomu na umwagaji wa tindikali ikiendelea mahakamani.

Kuimarishwa kwa ulinzi huo kulikwenda sambamba na ukaguzi kwa kutumia vifaa maalumu vya kutambua vitu vyenye chuma kwa watu walioingia eneo la mahakama.

Katika eneo hilo ndugu, jamaa na marafiki wa watuhumiwa 19 walionekana kufurika, lakini hata hivyo kutokana na ulinzi mkali watu hao hawakuruhusiwa kuingia mahakama ya wazi yalipokuwa yakisomwa mashtaka ya ndugu zao.

Ilipofika saa 4:30 asubuhi watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani wakiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi waliokuwa na magari zaidi ya 9 zikiwamo pikipiki za polisi.

Katika eneo la mahakama wakati watuhumiwa hao wakishushwa, ulinzi uliimarishwa zaidi kwa kila askari aliyekuwa eneo hilo akionekana kushika silaha yake tayari kwa tukio lolote litakalojitokeza.

Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi kuhusu ulinzi huo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, hakuweza kueleza idadi kamili ya askari waliomwagwa mahakamani hapo, ingawa alikiri uwepo wa askari wengi.

“Siwezi kukuambia walikuwa askari wangapi, hilo ni suala letu la ndani, itoshe kufahamu kwamba, tuliimarisha ulinzi vya kutosha na hii ni kutokana na na aina ya kesi yenyewe,” alisema.

Mashtaka

Akisoma mashtaka jana mbele ya Hakimu Mkazi, Devotha Msofe, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Augustino Kombe, alidai kuwa watuhumiwa, Yussuph Ally Huta (30) na wenzake 12 wanatuhumiwa kwa kesi ya ugaidi nyumbani kwa Sheikh Sudi Ally Sudi Julai 3, mwaka huu.

Kombe aliwataja watuhumiwa wengine katika kesi hiyo kuwa ni Abashar  Omar(24), Kassim Ramadhan,(34), Jafar Lema(38), Abdul Mohamed Humud (30), Said Temba (42), Idd Yusuph (32), Hassan Mfinanga (57), Anwar Nasher Hayel (29), Yahaya Twahir (37), Yusuph Ally Ramadhan (23) na Majid Michael.

Kombe alidai kuwa watuhumiwa wote wanadaiwa kufanya njama za kufanya vitendo vya kigaidi kati ya Januari na Februari mwaka huu, kwa kufanya njama ya ugaidi nyumba ya Sheikh Sudi.

Katika kosa la pili alidai watuhumiwa hao wanadaiwa kufanya ugaidi ambapo Julai 3 mwaka huu, katika eneo la Majengo mjini Arusha walirusha bomu la mkono na kumjeruhi, Sheikh Sudi na Muhad Hussein.

Akisoma shtaka la nne alidai kuwa linawakabili mtuhumiwa, Yahaya, Lema, Abdulmohamed na Temba wanaodaiwa kutoa ushirikiano uliosababisha kufanyika kwa kitendo cha kigaidi ambapo wanadaiwa kutoa msaada wa fedha kati ya Januari na Julai mwaka huu.

Washtakiwa bomu la Soweto

Mwendesha Mashtaka wa Serikali alidai katika kesi hiyo ya mauaji na kujaribu kuua inawakabili watuhumiwa 13.

Aliwataja watuhumiwa katika kesi hiyo kuwa ni Yusuph Huta (30), Yahaya Twahir (37), Jafar Lema (38), Ramadhan Waziri (28), Kassim Ramadhan (34), Abdul Mohamed Humud (30), Abashar  Omar (24), Abdulrahman Hassan (41), Morris Muzi (44), Miganya Miganya (28), Baraka Bilango (40), Hassan Omar na Said Temba.

Akisoma maelezo ya watuhumiwa hao alidai kwamba, kwa pamoja washtakiwa wote waliwaua, Judith Mushi, Ramadhan Juma, Fahad Jamal na Amir Daffa.

Kombe aliiambia Mahakama kuwa katika kesi hiyo watuhumiwa hao walijaribu kuwaua, Agustino Theodory, Sylvester Jakaranda, Abdallah Halela, Peter Mshanga, Raphael Mohamed, Emanuel Lucas, Abraham Shangwe na Patrick George.

Washtakiwa wakukutwa na mabomu

Mwendesha Mashtaka Kombe aliendelea kueleza kuwa kesi ya kukusanya zana, kukutwa na zana na kusamabaza zana kwa lengo la kufanya ugaidi inawakabili watuhumiwa 10.

Mwendesha Mashtaka Kombe aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Yussuph Huta, (30), Hassan Omar (40), Miganya Miganya (28), Sumaiya Ally (19), Morris Muzi (44), Hassan Mfinanga (57), Abashar  Omar(24), Ramadhan  Waziri (28) na Kimolo Issa.

Kombe alidai kuwa katika kosa la kukusanya zana na kutenda ugaidi ambapo watuhumiwa hao wanadaiwa kukusanya mabomu mawili kati ya Juni 23 hadi Julai 22 Mwaka huu kwa lengo la kufanya ugaidi.

Watuhumiwa wa tindikali

Mwendesha mashtaka wa Serikali, Marselino Mwamunyange, aliiambia mahakama hiyo kuwa washtakiwa wanne wanakabiliwa na kosa la ugaidi.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Kasssim Ramadhan (34), Jafar Lema (38) na Hassan Mfinanga (57).

Akielezea maelezo ya kosa hilo, Mwendesha Mashtaka Mwamunyange alidai kuwa watuhumiwa hao wanadaiwa kufanya kitendo cha ugaidi katika eneo la Msikiti Mkuu wa Arusha cha kummwagia tindikali Mustapha Kiago na kumsababishia majeraha mwilini.

Mwendesha Mashtaka Mwamunyange alidai kuwa katika kesi hiyo watuhumiwa wanashtakiwa kwa makosa ya ugaidi na kutenda njama ya kufanya ugaidi.

Aliwataja washtakiwa hao kuwa ni Yusuph Huta (30), Ramadhan Waziri (28), Kassim Ramadhan (34) na Jafar Lema(38), ambao kwa pamoja wanadaiwa kufanya kitendo cha kigaidi kwa kummwagia tindikali Sheikh Juma.

Mwamunyange alidai kwamba, kosa jingine linalowakabili ni kutenda njama ya kufanya ugaidi ambapo wanadaiwa kati ya Julai 2009 hadi Julai 2013 watuhumiwa hao walitenda kosa la kusababisha majeraha.

Watuhumiwa wa bomu

Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Felix Kwetukia alidai mahakamani hapo kuwa watuhumiwa katika kosa la kufanya ugaidi nyumbani kwa Abdulkarimu Jonjo ni Yussuph Huta (30), Kassim  Ramadhan (34), Mustapha Kiago (49) na Abdulaziz Mohamed (49).

Alidai kuwa watuhumiwa hao wanadaiwa kufanya njama za kutenda kosa hilo kati ya Oktoba mosi hadi Oktoba 25 mwaka 2012.

Kwetukia alidai kuwa kosa la pili kwa watuhumiwa hao ni la kufanya vitendo vya kigaidi ambapo wanadaiwa kufanya kosa la kutupa bomu lililotengenezwa kienyeji na kumjeruhi Sheikh Jonjo ambapo kosa la tatu ni la kufadhili na kuwezesha vitendo vya kigaidi kufanyika.

Ushawishi wa ugaidi

Mwendesha Mashtaka wa Serikali Kombe katika mashtaka hayo aliwataja watuhumiwa kuwa ni Ibrahim Lenard a.k.a Sheikh Abuu Ismail (37), Anwar  Hayel (29) na Yasini Shaban (20).

Alidai kuwa watuhumiwa hao wanadaiwa kati ya Machi 8 hadi Julai 14 mwaka huu waliwashawishi vijana kujiunga na kikundi cha kigaidi cha Al- Shabaab.

Mwendesha Mashtaka aliwataja waliosajiliwa kujiunga na kikundi hicho kuwa ni Abu Haris, Abu Shafy, Abu Mujahd, Soud Kabaju, Ahmed Islam, Mwinyi Mwinyi, Qassim Salaf na Rashid Salaf.

Kwa upande wake Hakimu Mkazi Msofe aliwataka watuhumiwa wote wasijibu chochote kwani mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hizo.

“Washtakiwa hamtakiwi kujibu chochote kwani Mahakama hii haina mamlaka ya kusikiliza kesi zinazowakabili na mtaendelea kukaa chini ya ulinzi kwani kesi hizi hazina dhamana,” alisema Msofe.

Upelelezi wa kesi zote bado haujakamilika na upande wa mashtaka waliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa ambapo kesi hizo zitatajwa tena Agosti 15, mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

2 COMMENTS

  1. Nguvu ya Mungu imeanza kufanya kazi. Sasa mambo yameanza kufunuliwa. Watu wamekufa na kujeruhiwa kwa muda mrefu, na watu wamepiga kelele juu ya makambi ya kujifunzia ugaidi hasa nyumba za ibada huko Arusha, lakini mara zote serikali ya CCM ilikuwa inakataa. Sasa hii ni nini kama siyo aibu, hawa watu wanafugwa na serikali, inajigamba kuwa na inteliigensia ya hali ya juu lakini mbona inachukua muda kubaini mambo? Na Hili ni janga kwa serikali ya JK awamu hii ya nne. Na kwa nini majina karibu yote ayanaonekana ni kama ya wafuasi wa dini moja kubwa hapa nchini? Hili nalo linatak kutuambia nini? Kwa kweli serikali hii inachezea amani na maisha ya Watanzania, je kuna uhallali wa kuendelea kuichagua tena? Suala la ulinzi kwa serikali yeyote ile ni wajibu namba moja, sasa kama usalama wetu upo mashakani hivi sijui serikali yetu inatupeleka wapi? Haya ni maswali ya kujiuliza tunapoelekea katika kipindi cha uchaguzi wa serikali za mitaa na ule uchaguzi mkuu wa mwakani (2015). Watanzania kama tuna akili timamu yatupasa kufikiri mara tano juu ya usalama wetu na wa vizazi vijavyo.

  2. Acha kuitupia lawama zisizo na msingi serikali.Wewe na wengine wa aina yako ni sehemu ya serikali, na unapaswa kuisaidia serikali kwa kutoa taarifa za kihalifu kama hizo,maana watu hao mnakaa nao mitaani na mnaona nyendo zao za kihalifu lakini hamsemi.Vyombo vya dola vitajuaje kila kitu kama si kwa msaada wa wananchi?Tuwe na uzalendo!

    Unapodai kwamba majina yote ni ya watu wa imani moja tu,ni kwamba hao ndiyo wahalifu waliokamatwa kulingana na upelelezi.Huwezi kuwakamata watu wa imani ingine eti ndiyo haki iwe imetendeka.Andika vitu vilivyosoma na si kuandika porojo ili tu na wewe uonekane mtandaoni.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles