UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umesema wapambe na vigogo waliompigia debe na kumnadi Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein kuwania urais mwaka 2010, hivi sasa wamemgeuka na hata baadhi yao kumuona kikwazo.
Kwa mujibu wa Umoja huo, vigogo hao sasa wamemgeuka na baadhi yao wanamuona kikwazo kwa msimamo wake wa mapinduzi na kuonekana mtu asiyeyumbishwa kwa kukataa vitisho.
Kauli hiyo ilitolewa mjini Unguja jana na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, alipozungumza na makundi ya vijana wa CCM kutoka majimboni ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya marudio ya uchaguzi wa Zanzibar.
Alisema madalali hao wa siasa hawakujua kama Dk. Shein ni zao la mapinduzi huku wazazi wake wakiwa ni waathirika wa Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12 mwaka 1964.
“Laiti kama Dk. Shein asingelelewa, kuandaliwa na kukuzwa kwa misingi ya mapinduzi, mbayuwayu na mbweha wanaopania kuyatokomeza mapinduzi yetu wangepata mwanya wa kuukwapua urithi huo.
“Waafrika wenyeji wangerudi katika kutumikishwa kazi za uyaya na ukuli na kulipwa ujira mdogo tofauti na jasho wanalolitoa,” alisema Shaka.
Aliwataka Wazanzibari kuendelea kumuunga mkono Dk. Shein wakiamini kiongozi huyo si wakala wala dalali.
“Naona fahari kukitumikia chama changu nikiwa bado kijana, nakomazwa, kufunzwa na kuelimishwa kujua pumba na mchele. Wanaojifanya vinara wa uongo nawasikitikia kwa sababu watamalizika kwa aibu katika siasa,” alisema.