32.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Jafo aagiza mkuu wa mkoa kuunda tume kukagua miradi

Amina Omari -Muheza

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais -Tamisemi, Selemani Jafo, amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigella kuunda tume itakayochunguza matumizi ya fedha katika ujenzi wa mradi wa Hospitali ya Wilaya ya Muheza ndani ya wiki mbili.

Hatua hiyo imekuja baada ya kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa hospitali hiyo, huku zaidi ya asilimia 80 ya fedha zikiwa zimetumika katika ujenzi.

Jafo alitoa maagizo hayo baada ya kufanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa hospitali hiyo juzi, ambayo ilitakiwa kukamilika tangu Agosti 30, mwaka huu.

“Kwa kweli Muheza sijaridhishwa na kasi ya ujenzi, hivyo natoa mpaka Oktoba 15 majengo haya yawe yamekamilika, bila hivyo nitazuia nyongeza ya fedha nyingine kwa ajili ya kumaliza miundombinu mingine katika hospitali hii,” alisema Jafo.

Kutokana na kutoridhishwa na kasi ya ujenzi huo, Jafo alilazimika kutoa tena muda wa wiki tatu kwa halmashauri hiyo kuhakikisha wanamalizia ujenzi wa majengo katika hospitali hiyo.

“Nilitoa muda wa kwanza wa hospitali za wilaya kumalizika mwanzoni mwa Juni, mara ya pili Agosti, lakini nyie mkaomba tena muongezewe muda. Sasa mpaka Oktoba 15 majengo yawe yamekamilika,” alisisitiza Jafo.

Alisema Serikali inajenga hospitali za wilaya kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya katika maeneo yao, lakini ucheleweshaji huo unasababisha kukosa huduma huku fedha ikiwa imepotea.

Awali msimamizi wa mradi huo, Ramadhani Mtinge, alisema majengo hayo tayari yametumia Sh bilioni 1.3 kati ya Sh bilioni 1.5 zilizopelekwa na Serikali.

Alisema changamoto ya miundombinu ya barabara pamoja na mafundi, imekuwa ni sehemu ya mradi huo kushindwa kukamilika kwa wakati.

Mbunge wa Muheza, Balozi Adadi Rajab aliiomba Serikali kupeleka fedha kwa ujenzi wa kituo afya cha Amani kutokana na uhitaji mkubwa uliopo.

“Mheshimiwa waziri, wananchi wa Kata ya Amani wanalazimika kutembea umbali wa kilometa 35 kufuata huduma ya afya, hivyo tayari wameshaanza ujenzi kwa nguvu zao, hivyo niombe Serikali ituunge mkono katika juhudi hizo,” alisema Balozi Adadi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles