31.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 10, 2024

Contact us: [email protected]

Wananchi Tanga wataka watendaji wabanwe kuruhusu ujenzi holela

Oscar Assenga -Tanga

SERIKALI imeombwa kuwachukulia hatua watendaji kwa kufumbia macho ujenzi holela, hasa maeneo ya taasisi za kiserikali na kusababisha wananchi hao kuvunjiwa makazi yao na kupata hasara.

Ombi hilo lilitolewa jana na Mbunge wa Tanga, Alhaji Mussa Mbaruku  (CUF) wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwatembelea wahanga walioathirika na bomoabomoa ya nyumba zaidi ya 200 zinazotakiwa kubomolewa kwa madai zimejengwa ndani ya eneo la uwanja wa ndege.

Mbaruku alisema maamuzi ya uchukuliwaji wa hatua za kinidhamu kwa watendaji hao yatasaidia kunusuru maeneo ya taasisi, hifadhi za Serikali.

Alisema wananchi wanajenga maeneo hayo bila ya kujua, huku watendaji wanaosimamia urasimishaji wa viwanja toka mashamba hadi makazi wakitambua uhalali wa maeneo hayo.

Mbunge huyo alisema ni jambo la kushangaza kuona nyumba zaidi ya 200 zikitakiwa kubomolewa wakati wamiliki wake waliuziwa maeneo hayo na watendaji wa halmashauri na kuweza kurasimishwa na kuendelea na ujenzi huku akitaka waliohusika na uuzaji maeneo hayo kwa wananchi wawajibishwe.

Aidha, alisema maamuzi magumu yanayochukuliwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) Mkoa wa Tanga hayana tofauti na yaliyotokea kwa Shirika la Reli kupitia Rahaco ambao walitaka kuvunja nyumba na hoteli kwa madai ya kuvamiwa maeneo yao.

Awali, wakizungumza mbele ya mbunge huyo, wamiliki wa nyumba hizo zilizopo eneo la Sinza Majonjo jijini hapa, walisema kinachofanywa na mamlaka hiyo ni unyanyasaji na ukatili wa hali ya juu kubomoa nyumba zenye thamani bila ya kujali maisha yao baada ya ubomoaji.

Katibu wa Kamati ya Ardhi Serikali ya Mtaa wa Njombe Mpirani, Kata ya Masiwani Shamba, Mfundo Silaha, alisema kila jambo lina utaratibu wake na ni kitu cha kushangaza kuona ubomoaji nyumba za wananchi huku mamlaka ya viwanja vya ndege inao maofisa wanaoweza kudhibiti maeneo yao.

 Silaha alisema nyumba zaidi ya 200 haziwezi kujengwa kwa siku moja na ndiyo maswali ya watu wengi kuhusu ujenzi wa makazi hayo haukuonekana na kudhibitiwa mapema hadi kufikia hatua ya kuwatia wananchi hasara na wengine kudaiwa kulazwa kwa mshutuko wa kubomolewa nyumba zao.

 “Napata shaka na viongozi wetu wa mkoa na wilaya, tangu ubomoaji wa nyumba uanze hakuna kiongozi yeyote aliyefika japo kwa kuwapa matumaini wananchi hawa ambao kesho ndio wapigakura wao, tupo kama yatima, nyumba zimevunjwa na watu wanalala nje sasa,” alisema Silaha.

Mkazi wa eneo hilo, Amina Hassan, alisema wanashangazwa na Serikali ambayo inadai kuwahurumia wananchi wanyonge wa hali ya chini huku ikiendelea kutekeleza azma yao bila kuwa na huruma kwa kuwakosesha makazi wananchi na familia zao huku wasijue cha kufanya.

Alisema ikiwa wenyeviti wa Serikali za mitaa wanapiga mihuri baadhi ya stakabadhi kwa viwanja hivyo ilihali wanajua maeneo hayo si salama, Serikali inapaswa kuwaadhibu badala ya kuwaonea wananchi wengine ambao labda hawajui chochote kuhusiana na uwanja huo wa ndege.

 “Ikiwa tunapata hadi stakabadhi toka Serikali za mitaa, maana yake wanatambua kama tunataka kujenga makazi, hivi ni kweli nyumba zote hizi zaidi ya 300 tangu zinajengwa hakuna kiongozi aliyeona na wakaweza kuzuia hadi watubomolee? Huu ni unyanyasaji wa hali ya juu,” alisema Hassan.

Hata hivyo, aliziomba mamlaka za juu kufika katika maeneo hayo na kuzungumza na wananchi ambao hawajui cha kufanya na waweze kuhojiwa utaratibu gani ulifuatwa wa upatikanaji wa viwanja hadi kufikiwa kujenga makazi yao ya kudumu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles