Gaudence Msuya-Kibiti
WATU wanne wakazi wa Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani, wamejeruhiwa jana baada ya kuzuka mapigano ya wafugaji na wakulima.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Rufiji, Onesmo Lianga, tukio hilo lilitokea Kijiji cha Lualuki wilayani Kibiti saa tatu asubuhi na kujeruhi watu wanne na mifugo 12.
Kamanda Lianga alisema majeruhi wote wamelazwa Hospitali ya Mchukwi Mission na mmoja kati yao yupo chumba maalumu cha uangalizi wa daktari kutokana na hali yake kuwa mbaya zaidi.
Alilaani tukio hilo na kusema Jeshi la Polisi litahakikisha kila aliyehusika na uovu huo anakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria ili iwe fundisho kwa watu wasioheshimu taratibu, kanuni na sheria za nchi.
Mtendaji wa Kijiji cha Lualuki, Fatuma Kangajao, alieleza hatua za awali zilizochukuliwa baada ya vurugu hizo ni kutoa taarifa polisi, lakini kabla hawajafika askari eneo la tukio, vijana wa wakulima waliamua kulipiza kisasi kwa kukatakata mifugo ya wafugaji hao.
Mmoja wa majeruhi, Rajab Zuber, akielezea tukio hilo lilivyotokea, alisema wafugaji waliingiza mifugo yao mashambani na walipowataka kuiondoa walikataa na ndipo yalipozuka mabishano na hatimaye wakapigwa kwa kutumia fimbo.
Mkulima Seleman Njegele naye alisema wafugaji hao walitumia silaha za jadi aina ya fimbo kuwacharaza wakulima ambao walikuwa wanatetea mazao yao yasiliwe na ng’ombe wao.
Mwenyekiti wa wafugaji Kijiji cha Lualuki, Maro Wangese, alieleza tukio hilo limetokana na ng’ombe wa wafugaji kuingia kwenye mashamba ya wakulima. Alisema baada ya ng’ombe kuingia katika mashamba ya wakulima yalizuka malumbano baina ya pande zote mbili yaliyosababisha mapigano.
Wangese licha ya kulaani tukio hilo, lakini pia aliahidi kulifuatilia na kuhakikisha haki inatendeka na kuchukua hatua kwa yeyote aliyehusika na vurugu hizo ili kuwafanya watu waheshimu sheria zilizopo.
Wananchi wa Kijiji cha Lualuki wameitaka Serikali kuchukua hatua za makusudi kukomesha vitendo vya kikatili vinavyofanywa na wafugaji dhidi ya wakulima ili kuwapa uhakika wa maisha yao wenye mashamba katika maeneo hayo tofauti na sasa hali si salama kwao.