25.5 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Waziri ataka wataalamu wajadili changamoto sekta ya anga

CHRISTINA GAULUHANGA Na

 CHELSEA TILLYA (UDSM)

DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isaack Kamwelwe, amewaagiza wataalamu wa Shirikisho la Kimataifa la Huduma za Anga na Uongozaji Ndege (CANSO), kujadili changamoto zilizopo katika sekta ya usafiri wa anga na kuzitafutia ufumbuzi ili kuchagiza uchumi katika nchi wanachama.

Akifungua mkutano wa CANSO Dar es Salaam jana, Waziri Kamwelwe alisema kuwa takwimu zinaonyesha usafiri wa anga ni moja ya sekta zinazokua kwa haraka kote duniani na hasa barani Afrika.

“Matumizi ya ndege zisizo na rubani ‘drones’ na watumiaji wa vyombo vingine tofauti na ndege za abiria yameongezeka hivyo kuleta changamoto ya namna bora ya kutoa huduma za uongozaji ndege na huduma nyingine,” alisema Kamwelwe.

Alisisitiza matarajio ya kuongezeka kwa vyombo vya angani pamoja na mabadiliko ya haraka ya teknolojia katika usafiri huo kunaleta chagizo  kwa mamlaka husika  kuangalia namna bora ya kudhibiti safari za anga  na zile za kutoa huduma za uongozaji ndege ili kuendelea kulinda usalama wa sekta ya anga.

Aliwataka wajumbe hao kuhakikisha wanajadili njia bora na namna ya kufikia malengo hayo ambapo Serikali tayari imeanza kuchukua tahadhari ikiwa ni pamoja na kufunga rada nne zenye thamani ya Sh bilioni 67.3.

Alisema kaulimbiu ya mkutano huo “Kuelekea anga isiyo na mipaka barani Afrika na mchango wake katika kizazi kijacho cha wataalamu wa usafiri wa anga” ni sehemu ya uendelezaji jitihada za nchi za Afrika kuhakikisha mitambo inayotumika kutoa huduma za anga na uongozaji ndege anga la Afrika inafanana.

“Teknolojia zetu Afrika zikiondolewa vikwazo zikawiana, somana na kuingiliana, kutawezesha watumiaji wa anga kutohisi tofauti ya taratibu za matumizi ya anga anapotoka nchi moja kwenda nyingine, pia itasaidia kuboresha huduma na ufanisi,” alisema Kamwelwe.

Alisema Serikali inaendelea na jitihada ikiwamo ufungaji vifaa vya usalama katika viwanja vya ndege vya kimataifa, kuimarisha mifumo ya mawasiliano kwa kufunga mitambo ya radio mpya, kuteua viongozi wanaoweza, wenye weledi na kusomesha wataalamu wa fani mbalimbali na kulifufua  Shirika la Ndege Tanzania kwa kununua ndege mpya.

Mwenyekiti wa CANSO Afrika, Hamza Johari, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), alisema wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kadhaa katika sekta hiyo ambazo baadhi wameanza kuzifanyia kazi.

Alisema hadi sasa wameweka utaratibu wa uongozaji ndege ndogo ‘drones’  ili kupunguza ajali. Johari alisema kuna utaratibu maalumu umewekwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles