27.1 C
Dar es Salaam
Monday, September 25, 2023

Contact us: [email protected]

TCRA yashusha rungu kwa vyombo vya habari

KULWA MZEE – DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kupitia Kamati ya Maudhui imetoa onyo kali kwa Lemutuz Televisheni na Global Televisheni na kuamuriwa kuomba radhi kwa watazamaji kwa siku saba kwa kosa la kurusha na kuonyesha kwa uwazi miili ya watu waliofariki dunia baada ya kuungua moto katika ajali ya lori la mafuta iliyotokea Msamvu mkoani Morogoro.

Vyombo vingine vya habari vilivyopewa onyo kwa kukiuka kanuni ni East Africa Televisheni na TBC Fm waliokiuka agizo la Serikali kwa kusoma kwa undani habari mbalimbali katika magazeti ya Uhuru na Habari Leo.

Akisoma uamuzi wa kamati hiyo Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati, Valerie Msoka, alisema Agosti 10 mwaka huu taifa lilipata janga la kupoteza wananchi wake katika ajali ya moto uliohusisha gari la mafuta maeneo ya Msamvu mkoani Morogoro.

“Katika hali ya kusikitisha na kustaajabisha, baadhi ya vyombo vya habari hususan online TV zaidi ya 15 zilichapisha na kuonyesha picha mbalimbali za miili ya watu waliofariki katika ajali hiyo kinyume cha sheria, kanuni na maadili ya uandishi na utangazaji wa habari,” alisema.

Alisema baadhi ya vyombo vilibaini makosa na kuziondoa picha hizo kama ambavyo Kanuni ya 16 (1) na(2) ya Kanuni ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya mwaka 2018 inavyompa fursa aliyechapisha kuondoa ndani ya saa 12.

Msoka alisema viongozi wa Lemutuz na Global walifika katika kamati hiyo Agosti 28, mwaka huu na kujitetea kwamba kosa hilo lilisababishwa na uzembe wa msimamizi wa maudhui ambaye hakutumia busara na kuzingatia weledi katika uchapishaji wa video.

Walikiri kosa lao na kuomba wasamehewe.

Global walijitetea kwamba walichukua tahadhari kubwa ya kuziziba picha kwa kuwekea kivuli, lakini lilitokea tatizo la kiufundi na kuonyesha picha hizo chini ya kivuli.

Walisema chaneli haikuwa na nia ovu, walikiri kosa na kuomba radhi wakiahidi kutorudia.

“Baada ya kutafakari, kamati imeridhika kuwa Lemutuz na Global zimekiuka kanuni za mawasiliano ya kielektroniki na posta ya mwaka 2018 hivyo wamepewa onyo kali na wameamriwa kuomba radhi kwa watazamaji kupitia chaneli zao kwa siku saba mfululizo kuanzia Septemba 4, mwaka huu.

“East Africa Televisheni kupitia kipindi cha Dadas kwenye kipengele cha ‘Mtu kati’ walirusha maudhui yasiyo na maadili wala weledi yaliyohusu mambo ya watu wazima katika muda ambao watoto wanaweza kusikia kinyume cha sheria na kanuni za mawasiliano,” alisema.

Alisema kituo hicho kiliomba radhi na kamati ilikubali kwamba walikosea, hivyo imewapa onyo kali na kuwataka kuhakikisha watumishi wake wote wanazielewa na kuzifuata sheria na kanuni za mawasiliano.

“TBC FM Radio Agosti 2, mwaka huu saa 12 asubuhi na saa nne asubuhi walikiuka agizo la Serikali kupitia kipindi cha Busati ambapo mtangazaji alisoma kwa undani habari mbalimbali katika magazeti ya Uhuru na Habari Leo,” alisema Msoka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,717FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles