RAMADHAN HASSAN – DODOMA
CHAMA cha Wananchi (CUF), kimemtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Simon Sirro, kutekeleza agizo la Rais Dk. John Magufuli la kupiga marufuku mikutano ya vyama vya siasa bila kufanya upendeleo vinginevyo na wao wataanza kufanya mikutano nchi nzima.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho upande wake Bara, Maftaha Nachuma, alisema agizo hilo la Rais Magufuli halitekelezwi kwa usawa.
“IGP inabidi aliangalie hili kwani agizo la Rais Magufuli ni kwa vyama vyote vya siasa nchini na siyo wao kuendelea kufanya mikutano katika maeneo yao lazima haki izingatiwe kila chama kina haki zake za msingi kwamujibu wa sheria ya vyama vya siasa,” alisema Nachuma.
Alisema kama jeshi la polisi litaendelea kukilea chama cha CCM na kukiachia kuendelea kufanya mikutano ya kisiasa katika maeneo mbalimbali na wao pia wataanza kufanya mikutano kwa kuzunguka nchi nzima.
“Leo hii tulikuwa tufanye mkutano wa chama chetu katika maeneo la Vingunguti jijini Dar es saalam lakini jeshi la polisi limetukataza na kusema kuwa hilo ni agizo la Rais Magufuli lakini wenzetu CCM wanajiandaa tarehe 31 mwezi huu watakuwa na mkutano kule Mtwara na mageni rasmi atakuwa Mzee Pinda (Waziri Mkuu mstaafu),” alihoji Nachuma.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana wa CUF, Hamidu Bobali, alisema hivi sasa CCM imekuwa ikifanya mikutano yao kwa kutumia ujumbe wa Tanzania ya Kijani.
Bobali alisema mikutano hiyo ambayo CCM wamekuwa wakiifanya wakihoji wanadai kuwa wanakwenda kukagua utekelezaji wa ilani ya chama chao.
“Kama wao wanakwenda kukagua utekelezaji wa ilani kwanini na sisi kule ambako kuna diwani wetu, mbunge wetu tusiruhusuwe kwenda kuona kuna ahadi zipi zimetekelezwa katika eneo hilo,” alisema Bobali ambaye pia ni Mbunge wa Mchinga.