Mwandishi Wetu -Tokyo
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Kampuni ya Toshiba nchini Japan.
Katika mazungumzo hayo, amewashawishi kuja na wafungue ofisi kubwa ili waanzishe viwanda vya bidhaa za elektroniki watakavyoona vinafaa hapa nchini.
Waziri Mkuu ameyasema hayo jana, baada ya kutembelea makumbusho ya sayansi ya Toshiba na kiwanda cha kutengeneza mitambo ya kuzalisha umeme cha Tsurumi kinachomilikiwa na kampuni hiyo.
Aliwashawishi waje nchini na wafungue viwanda vya kutengeneza bidhaa mbalimbali za elektroniki kama vile redio, televisheni, pasi na viwanda vingine watakavyoona wao vinafaa kujengwa nchini.
Aliwahakikisha hawatojuta kuwekeza Tanzania kutokana na sera nzuri na mazingira mazuri ya uwekezaji.
“Wawekezaji wote wanaokuja kuwekeza Tanzania, wakiwemo wa kutoka Japan na Kampuni ya Toshiba, watambue Serikali imeboresha mazingira ya uwekezaji na kuyafanya yawe rafiki, nina uhakika wawekezaji watakaoamua kuwekeza Tanzania hawatajutia uamuzi wao huo”.
Alisema ujio wa kampuni kubwa utawapa Watanzania fursa ya kujifunza teknolojia mpya na namna bora ya uendeshaji wa biashara unaozingatia viwango vya kimataifa.
Mkurugenzi wa Makumbusho ya Sayansi ya Toshiba, Takano Lwakiri, alimwambia Majaliwa kampuni yake iko tayari kupanua ofisi yake ya Tanzania na kufungua biashara, na ameomba yafanyike mazungumzo yatakayotoa dira sahihi ya kufanikisha jambo hilo.
Kuhusu mkutano wa Saba wa Tokyo International Conference on Africa Development (TICAD 7), utakaoanza leo jijini Yokohama, alisema anaamini utakuwa na mafanikio makubwa kutokana na ajenda zilizoandaliwa.
Lwakiri alisema miongoni mwa ajenda zitakazojadiliwa ni namna ya kuunganisha kibiashara shughuli za Serikali na sekta binafsi.
Alisema kwa kutumia mkutano huo, wafanyabiashara wa Tanzania wanayo fursa ya kunufaika kwa kuunganisha nguvu zao na kampuni kubwa za nchini Japan.