25.8 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Vifo ajali lori la mafuta vyafikia 102

AVELINE KITOMARY NA SAID IBADA (TUDACo)-DAR ES SALAAM 

MAJERUHI mmoja kati ya 14 wanaoendelea kutibiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), amefariki dunia na kufanya idadi ya waliopoteza maisha katika ajali ya lori la mafuta iliyotokea Agosti 10 mkoani Morogoro kufikia 102.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma wa MNH, Aminiel Aligaesha, alimtaja majeruhi aliyefariki dunia ni Grayson Ndabita (23).

Aligaesha alisema kati ya majeruhi 47 waliofikishwa katika hospitali hiyo, wamebaki 13.

Alisema majeruhi saba wako katika vyumba vya uangalizi maalumu (ICU) na sita katika wodi za jengo la Sewahaji.

“Majeruhi mmoja amefariki dunia tarehe 23 saa saba mchana na sasa wamebaki majeruhi 13 kati ya wale 47 waliofikishwa hapa Muhimbili,” alisema Aligaesha. 

Alisema jumla ya majeruhi waliofariki wakiwa wanatibiwa Muhimbili imefikia 34.

Aligaesha alisema majeruhi sita walioko Sewahaji afya zao zinaendelea kuimarika na wanaendelea kufanya mazoezi. 

“Majeruhi sita waliopo katika wodi za kawaida jengo la Sewahaji wanaendelea vizuri na afya zao zinaendelea kuimarika na wanaendelea kufanya mazoezi,” alieleza Aligaesha.

Alisema majeruhi walioungua moto matibabu yao yanahitaji muda mrefu, hivyo wataendelea kuwahudumia hadi watakapofanikisha matibabu yao yote.

“Matibabu yao yana mchakato, akisoma hapa kuna kufanyiwa upasuaji halafu pia wataalamu wa saikolojia wanahitajika kumuweka mgonjwa vizuri kisaikolojia watakapopona,” alisema Aligaesha. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles