25.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 10, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri aagiza wakandarasi wakamatwe

Mwandishi Wetu -Katavi

WAZIRI wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, ameagiza vyombo vya usalama mkoani Katavi kuwakamata wakandarasi wa Kampuni ya China Railways Construction Electrification Bureau Group Co Ltd (CRCBEG) baada ya kusuasua kusambaza umeme vijijini.

Waziri Kalemani, alimwagiza Kamanda wa   Polisi Mkoa wa Katavi, Benjamin Kuzaga  kushikilia hati za kusafiria za raia wawili wa China ambao ni wakandarasi wa kampuni hiyo, baada ya kutoridhishwa na kasi yao ya usambazaji na uwashaji umeme vijijini (REA)  awamu ya tatu.

Pia aliagiza wakandarasi wote wa kampuni hiyo wanaofanya kazi ya mradi huo, lakini wanaishi Dar es Salaam badala ya Katavi warudi haraka kuendelea na kazi.

Maagizo hayo yalitolewa jana wakati Waziri Kalemani alipohutubia wakazi wa Kijiji cha  Sosayati, Manispaa ya Mpanda, baada ya kuzindua na kuwasha umeme.

Alisema hafurahishwi na utendaji kazi wa  kampuni hiyo iliyopewa jukumu la kusambaza umeme Mkoa wa Katavi kutokana na kuwa na kasi ndogo ya utekelezaji.

 “Nilitoa mwezi mmoja eneo lote la kilometa 27 muwe mmeshawashiwa umeme, lakini mpaka sasa bado, Kijiji cha Majimoto hamjawashiwa, nimepita hapa sijaona vibarua wakihangaika wala nguzo hazijafika, nimefika shule ya sekondari kule nguzo hazijafika na wala hamjasambaza popote,” alisema Dk. Kalemani.

Pia aliwaagiza mameneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kutoondoka eneo hilo ili kuhakikisha kazi ya usambazaji umeme inafanyika kwa kasi zaidi.

“Nataka umeme ufike Kijiji cha Majimoto ifikapo Septemba 5, mameneja wote mtabaki hapa kusimamia kazi,” aliagiza.

Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ntibiri, alisema Serikali imetoa Sh bilioni 89 kwa usambazaji umeme mkoani hapa.

Akiwa wilayani Mlele, aliwasha umeme katika Kijiji cha Society eneo la wachimbaji wadogo wa dhahabu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles