HASSAN DAUDI NA MITANDAO
WAKATI Uchaguzi Mkuu ukitarajiwa kufanyika kuanzia Novemba 9 na kumalizika Desemba 9, mwaka huu, gumzo kubwa nchini Sri Lanka ni kitendo cha upinzani, People’s Front, kumtangaza mgombea wao kuwa ni Mkuu wa Majeshi wa zamani nchini humo, Gotabhaya Rajapaksa. Bado Chama tawala, United National Party (UNP), hakijamtangaza mgombea wake.
Kwa wafuatiliaji wa siasa za Sri Lanka, watakumbuka kuwa miaka 10 iliyopita, Rajapaksa alisimamia kwa ukamilifu operesheni ya kutokomeza waasi mjini Tamil wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe. Jumla ya watu 100,000 walitajwa kupoteza maisha wakati wa vurugu hizo.
Serikali ya sasa ya Sri Lanka, chini ya UNP inayoongozwa na Rais Maithripala Sirisena na Waziri Mkuu wake, Ranil Wickremesinghe, inakabiliwa na changamoto kubwa ya mauaji ya kujitoa muhanga, yanayofanywa na vikundi vya Kiislam, likiwamo tukio baya zaidi la hivi karibuni lililoacha vifo vya watu 253.
Idadi kubwa ya wananchi wa Sri Lanka hawaoneshi kufurahishwa na namna mambo yanayokwenda, hasa Serikali yao kushindwa kumaliza tatizo la mashambulio ya kujitoa muhanga. Hasira za walio wengi ni kwamba, Serikali yao imeshindwa kupunguza kama si kutokomeza kabisa mashambulio ya kujitoa muhanga, ambayo yamekuwa yakigharimu maisha ya wananchi.
Licha ya Umoja wa Mataifa (UN) kuitaka Serikali ya Sri Lanka kufanya uchunguzi, bado hakuna kilichofanyika, viongozi walioko madarakani wakisema hayo ni mambo ya ndani hivyo, hayatakiwi kuingiliwa. Ni kutokana na hali hiyo basi, wananchi wa taifa hilo wanataka kuona uongozi ujao ukiwa imara zaidi kuliko huu wa sasa wa Rais Sirisena.
Hata hivyo, huku ikionekana labda wananchi hawakunwi na mwenendo wa serikali yao, ukweli ni kwamba bado upinzani una kibarua kizito kwa kumteua Rajapaksa kupeperusha bendera yao kwa kuwa hata Mkuu wa Majeshi huyo wa zamani anakabiliwa na kashfa mbalimbali.
Akiwa Waziri wa Ulinzi, kuanzia mwaka 2005 hadi 2015, wengi hawajasahau kwamba Rajapaksa alikuwa mmoja kati ya viongozi waliokuwa wakisifika kwa matukio ya uvunjifu wa haki za binadamu. Ni kipindi ambacho kaka yake, Mahinda Rajapaksa, alikuwa rais wa taifa hilo.
Kutokana na amri zake, waandishi wa habari, hasa waliokuwa wakipingana na utendaji kazi wa Serikali, walikuwa wakikamatwa, wakiteswa na hata kuuliwa, ukiacha waliokuwa wakipotea bila kuwapo kwa taarifa za kueleweka.
Ni kipindi hiki, Rajapaksa alitajwa kuwa mtu mwenye hasira, hata waandishi wa habari wakishindwa kumuuliza maswali magumu, hasa yaliyolenga kuhoji uvunjifu wa haki za binadamu uliokuwa ukifanywa na vyombo vya dola nchini Sri Lanka.
Hofu nyingine dhidi yake kuelekea Uchaguzi Mkuu huo wa mwishoni mwa mwaka huu, ni kesi nyingi zinazomkabili katika mahakama za huko Marekani. Kwanza, unaweza kuikumbuka ile ya Aprili, mwaka huu, akishitakiwa kwa mauaji ya mhariri wa gazeti la Sunday Leader la Sri Lanka, Lasantha Wickrematunge. Ni miaka 10 imepita tangu kutokea kwa tukio hilo.
Wickrematunge ni mmoja kati ya waliokuwa wahariri maarufu zaidi ndani ya taifa hilo, ambaye wengi wanakumbuka namna alivyokuwa mstari wa mbele kukosoa utendaji kazi wa Serikali iliyokuwa madarakani. Sehemu kubwa ya maandiko yake yalihusu namna viongozi waliokuwa madarakani, hasa Wizara ya Ulinzi iliyokuwa chini ya Rajapaksa, walivyokuwa wakijihusisha na vitendo vya rushwa.
Kabla ya kuibuka kwa taarifa za kifo chake, ambazo ziliwashtua walio wengi, Wickrematunge alipokea taarifa za vitisho kutokana na tabia yake ya kuikosoa serikali. Zaidi ya hapo, aliwahi kuandika katika moja ya tahariri zake kwamba ipo siku Serikali ya Sri Lanka itamuua.
Haikuchukua muda mrefu kwani Januari, 2009, aliuawa kwa kupigwa risasi na kuchomwa kisu mjini Colombo, waliotekeleza uhalifu huo wakibaki kuwa ni ‘watu wasiojulikana’. Hadi leo, ikiwa imebaki miezi michache kabla ya Uchaguzi Mkuu, hakuna aliyekamatwa kwa madai ya kuhusika na kifo cha mwandishi wa habari huyo.
Pia, ipo kesi inayomtaja kuhusika katika mateso makali waliyoyapata watu waliokuwa wameshikikiliwa wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe huko Sri Lanka miaka 10 iliyopita. Katika hilo, anayetajwa hapa ni Roy Samathanam, mwananchi wa Sri Lanka mwenye uraia wa Canada.
Samathanam alikamatwa akiwa Sri Lanka, akiingizwa katika orodha ya waasi, kabla ya kuachiwa mwaka 2020, ambapo baadaye alifichua mateso makali aliyopewa akiwa chini ya vyombo vya dola, akisema alikuwa akilazimishwa kukiri kosa hilo. Haiishii hapo kwani kesi dhidi ya Rajapaksa ziliendelea, ikiwamo ile ya waliowahi kushikiliwa chini ya utawala wake kudai kubakwa.
Katika hatua nyingine, licha ya makandokando yote hayo ya Rajapaksa, tayari wapo wanaomtaja kuwa ni ‘mtu aliyebadilika’ katika siku za hivi karibuni, hata kabla ya kutangazwa kuwa ndiye atakayeibeba bendera ya upinzani. Tofauti na ilivyokuwa awali, sasa wengi wanamuona kuwa ametulia katika majibu yake, hasa yanayohusu mustakabali wa taifa hilo.
“Nitapokea majukumu ya usalama wenu, usalama wa watoto wenu na mnaowapenda. Nafikiri nchi yoyote, serikali yoyote, au kiongozi yeyote anatakiwa kuwa makini katika suala la usalama, hasa kipindi hiki, ambacho duniani kote kumekuwapo na matukio ya kigaidi,” anasema Rajapaksa akiwaambia waandishi wa habari mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Colombo.
Huku akikanusha tuhuma zote za awali, akisema zimejengwa kwa misingi ya kuichafua taswira yake kisiasa, aliwatoa shaka wananchi wa Sri Lanka watakaompigia kura akiwaambia: “Nimejipanga kuweka mazingira safi kwa wananchi wote wa Sri Lanka, bila kujali rangi wala dini, kuhakikisha wanaishi kwa amani na upendo.”
Akigusia kesi zinazomkabili nchini Marekani, anasema si kweli kwani zimejaa siasa, zikilenga kumtoa katika harakati zake za kwenda Ikulu. “Nimekuwa nikienda Marekani kwa miaka mingi, kwanini hilo limeibuka kipindi hiki?”