ALOYCE NDELEIO
TANZANIA imekuwa mwenyeji wa Mkutano wa 39 wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) inayoundwa na nchi 16.
Msisitizo mkubwa katika mkutano huo umekuwa ni suala la kukuza ushirikiano wa kiuchumi miongoni mwa nchi hizo ikiwa ni mkakati wa kuziwezesha kuingia katika uchumi wa kati, hususani kukuza sekta ya viwanda, ili iwe nyenzo muhimu ya maendeleo.
Ushirikiano miongoni mwa nchi hizo unasadifu kuwa ni mwitiko chanya kwa maono ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipokuwa akizungumzia majukumu ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere akisema: “Mimi bado ni muumini kwamba vi-nchi vyetu ni vidogo mno; mkiendelea navyo hamuendi mbali.
“Lazima mjitahidi kuziunganisha nchi zetu…Dunia inayokuja si ya huruma na si ya mchezo mchezo…Mashindano yake yatakuwa ni makali sana hivyo, ni lazima mjenge nguvu. Vi-Tanzania hivi, Vi-Kenya hivi, Vi-Zimbabwe peke yao havina nafasi katika dunia hiyo.”
Pamoja na kuwapo kwa jumuiya nyingine za maendeleo ndani ya Afrika, SADC ndiyo inaonekana kuwa na nguvu zaidi na inaweza kutoa mchango mkubwa katika nyanja mbalimbali ya maendeleo.
Ushirikiano miongoni mwa nchi hizo kwa kuzingatia kwamba dira ni kuwa na uchumi wa kati ukifungamana na viwanda, ni pamoja na kuwa na miundombinu ya kusafirisha bidhaa kutoka eneo moja hadi jingine.
Katika uhalisia wake, kigezo cha mazingira rafiki ndicho kitakachoonesha uwazi kuwa ushirikino ni muhimu kwa sababu utaziwezesha nchi kujenga uchumi wa pamoja na hivyo kupunguza vikwazo vya masoko vinavyoshinikizwa na masoko makubwa.
Vikwazo vya masoko makubwa vinaeleweka miongoni mwa viongozi wengi wa Afrika na wengine wameshalifanyia kazi suala la uchumi na kuona unyonyaji unaofanywa na mataifa ya nje.
Miongoni mwa viongozi hao ni pamoja na Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, ambaye nchi yake imo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na anasema kuwa hali hiyo itapunguza utegemezi wa misaada.
“Moja ya kichocheo kitakachotuwezesha kukua kiuchumi na mabadiliko ya kijamii ni kuyafikia masoko ya nchi tajiri.
“Misaada peke yake ni kitu kidogo na ni kama ishara tu, haiwezi kutatua matatizo ya kiuchumi ya nchi za Afrika. Kama ni misaada kwa ajili ya kuhamasisha uzalishaji na kuwezesha biashara hiyo ndiyo sawia.
“Nchi za Afrika zimepata uhuru miaka 50 iliyopita na zimekuwa zikipata misaada tangu wakati huo, lakini haijaleta mabadiliko kutoka kubakia nyuma na kusonga mbele.
“Ni uthibitisho gani tena unaoutaka kuonesha kuwa misaada haiwezi kuleta mabadiliko? Hata hivyo, biashara inaweza. Kama tukifanya kazi pamoja ni ndani ya uwezo wetu huo tunaweza kuboresha maendeleo endelevu.”
Anabainisha kuwa nchi zilizoendelea si tu kwamba zinazifanyia vibaya nchi nyingine zinazoendelea, bali pia zinawalaghai watu wao kwa kuwauzia bidhaa zinazotoka Afrika kwa bei ya juu zaidi.
“Mimi ni mfugaji wa ng’ombe wa nyama na ninauza nyama dola moja kwa kilo. Wafanyabiashara wanaonunua kutoka kwangu wanawatoza wateja wao dola mbili kwa kilo. Kilo ya nyama hiyo mjini London ni dola 17 na Japan ni dola 200.
“Niliwauliza watu hao ni nyama ya aina gani hiyo inayouzwa kilo moja dola 200. Wakanijibu ni kobe. Nikawauliza hiyo kobe ni nini? Wakaniambia kuwa unampigia ng’ombe muziki, unampa pombe halafu unampiga masaji. Hali hiyo inaifanya nyama yake kuwa nzuri zaidi,” anabainisha.
Anafahamisha kuwa nchi za magharibi zinawadanganya hata watu wake, kuwatoza zaidi na hivyo kudumaza kukua kwa uchumi kwa kutunyima masoko ya kuuza kile tunachozalisha.
“Kama wanachukua nyama kutoka kwangu kwa dola nne na kuiuza London kwa dola nane, ikijumuisha gharama za usafiri n.k. itakuwa ni vizuri zaidi kwa wote nchi za Ulaya na sisi,” anasema.
Kuongeza thamani ya bidhaa ni njia nyingine. Kichocheo kingine cha kukuza uchumi ni kuongeza thamani malighafi ambazo ndizo bidhaa ambazo Afrika inauza zaidi. Chukulia mfano wa kahawa: Kilo 2.5 za kahawa zinauzwa kwa dola 1.25, pindi ikikaangwa na kusagwa wanauza dola 70 kwa kilo. Kwanini tusifungashe, tukaikaanga na kuisaga hapa ndani? Upotevu huu mkubwa wa thamani ya bidhaa lazima usitishwe.
Aidha, ni katika mazingira hayo mkutano huo wa SADC utanguliwa na maonesho ya biashara na viwanda ya wiki moja ambapo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi (SMZ), Dk. Mohammed Shein, alipokuwa anafunga maonesho hayo alisema kuwa ili kufikia uchumi wa viwanda nchi za SADC zinatakiwa kuongeza ubora wa bidhaa katika utengenezaji na kushirikiana katika mnyororo wa thamani.