29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

DC aagiza mali za mwekezaji zizuiwe

Mary Mwita – Longido

MKUU wa Wilaya ya Longido, Franck Mwaisumbe, ameagiza Jeshi la Polisi kulinda kitalu cha Lake Natron East kilichokuwa kinamilikiwa na Kampuni ya Green Miles hadi mwekezaji huyo atakapolipa zaidi ya Sh milioni 336 ambazo ni fedha za vijiji 23.

Hatua hii, imekuja siku moja baada ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangalla kufuta leseni ya umiliki wa kitalu hicho na mali zake.

Taarifa ya Dk. Kigwangalla ilisema ametumia mamlaka aliyopewa kisheria.

Kutokana na hali hiyo, Serikali imeagiza mwekezaji huyo asipewe mali zake hadi alipe fedha anazodaiwa,  kwa kuziweka katika akaunti za vijiji husika.

Mwaisumbe alitoa agizo hilo jana mbele ya wananchi wa Tarafa za Longido, Engaranaibo na Kitumbeine,

Kijiji cha Mundarara walikokusanyika kusherehekea kufutwa kwa kitalu hicho.

Alisema fedha hizo ni za wananchi kutoka vijiji 23 ambao walikuwa jirani na kitalu hicho.

Mwaisumbe alisema wananchi hao wanamdai mwekezaji huyo kwa zaidi ya miaka minne na  kila kijiji kinamdai zaidi ya Sh milioni 14.

Alisema tayari mwekezaji huyo amefutiwa umiliki wa kitalu na haruhusiwi kuchukua mali katika eneo  hilo hadi atakapolipa fedha.

“Wananchi wamenyanyaswa vya kutosha, tunashukuru  Rais  Dk. John Pombe Magufuli kumfutia umiliki, wananchi wameondokana na unyonyaji,” alisema Mwaisumbe.

Diwani wa Kata ya Mundarara, Alaisi Ruben, akizungumza kwa niaba ya wananchi wa kata yake, alisema wamekombolewa kutoka makucha ya  unyonyaji na wanyama wao hawatauliwa ovyo.

Alishukuru jitihada zilizofanywa na uongozi wa wilaya wakishirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo,  ambazo zimemfanya Dk. Kigwangalla kuchukua uamuzi sahihi.

Alisema haki imetendeka kumfutia leseni Green Miles kwa kuwa alikiuka mkataba, ikiwa ni pamoja na kushindwa kulipa fidia jambo ambalo lilisababisha kukwamisha maendeleo.

Kwa upande wake, Peter Sengeyu (Laigwanani), alimpongeza Rais Magufuli na kusema amesikia kilio chao cha muda mrefu.

Sengeyu alisema wananchi walikuwa wanaonewa, huku wanyamapori wakiuawa ovyo.

Alisema wamefurahishwa na hatua ya kufuta umiliki na kuomba mali za mwekezaji huyo zishikiliwe hadi atakapolipa deni la kijiji.

Mwekezaji wa Kampuni ya Green Miles, alianza kuwekeza katika tarafa za Longido, Engaranaibo na Kitumbeine mwaka 2013.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles