23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Familia ya Lissu kudai haki ya matibabu mahakamani

Janeth Mushi -Arusha

FAMILIA ya aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), imeeleza nia yao ya kufungua kesi ya kudai haki za ndugu yao, ikiwemo gharama za matibabu aliyopatiwa nje ya nchi.

Kwamba Lissu atakaporejea nchini mwezi ujao kutoka nchini Ubelgiji anakotibiwa, atafuatilia haki zake.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha jana, msemaji wa familia hiyo Wakili Alute Mughwai, alisema Lissu anatarajiwa kurejea nchini Septemba 7.

Wakili Mughwai alisema Lissu ataenda kuonana na madaktari wake Agosti 20 kufanyiwa vipimo mara ya mwisho kabla kupewa ruhusa ya kuondoka hospitalini.

Alisema maandalizi ya ujio wake yanaendelea na kuwa taarifa zaidi zitaendelea kutolewa.

Wakili Mughwai alisema kwamba Lissu alishasema atakwenda mahakamani kudai haki zake, kwamba amekuwa akilalamika hakutendewa haki na ofisi ya Bunge ya kutokutibiwa kwa gharama ya mhimili huo, kama ambavyo alikuwa anastahili, pamoja na kulipwa posho akiwa hospitalini.

 “Nia yake ya kwenda mahakamani juu ya jambo hili bado ipo, na akirudi pamoja na mambo mengine atachukua hatua hiyo kufungua shauri mahakamani ili mahakama iweze kuamua kama madai yake kutibiwa kwa gharama za Bunge ni halali au hapana.

“Aidha kwa kupitia mahakamani, atauliza ofisi ya Bunge ni kwanini mpaka sasa hivi uongozi wa Bunge haujaanzisha bima kwa ajili ya matibabu ya wabunge nje ya nchi pale inapohitajika kwa mujibu wa sheria ya uendeshaji wa shughuli za Bunge ya mwaka 2008, sura ya 115 ambapo kifungu cha 24 cha sheria hiyo kinasema Bunge litaweka bima mahsusi kwa ajili ya mbunge.

“Mwenza wake au watoto wasiozidi wanne wenye umri chini ya miaka 18 haki ya kupata matibabu ndani na nje ya nchi, ila utaratibu wa sasa hivi wabunge wana bima ya kutibiwa ndani ya nchi, lakini hakuna bima yao ya kutibiwa kama itahitajika nje ya nchi, na ndiyo takwa la kisheria na wabunge wanaohitaji kutibiwa nje ya nchi inabidi wategemee huruma za watu wengine,” alisema Mughwai.

Alisema suala la pili atakalofuatilia Lissu ambaye alikuwa ni Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, ni kuweka msukumo wa tukio la Septemba 7, 2017 la shambulio la kujaribu kumuua akiwa nje ya makazi yake jijini Dodoma, ili uchunguzi wa tukio hilo ukamilike na watakaobainika kuhusika wafikishwe kwenye vyombo vya dola.

JOPO LA MAWAKILI

Kuhusu maombi ya Lissu kwa mahakama kuitaka kutengua tangazo la kumvua ubunge lililotolewa hivi karibuni na Spika wa Bunge, Job Ndugai, Mughwai alisema jopo la mawakili wanne; Peter Kibatala, Jeremia Mtobesia, John Mallya na Fred Kalonga wanatarajiwa kumwakilisha.

Alidai kuwa katika maombi hayo yaliyowasilishwa chini ya hati ya dharura, wajibu maombi ni Spika Ndugai na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Kwamba shauri hilo limefunguliwa na hati ya wito ambayo imeambatanishwa na maelezo na kuungwa mkono na hati mbili za viapo na vielelezo 27 ambavyo vinakamilisha maombi hayo.

Mughwai alidai kuwa maombi hayo yaliwasilishwa mahakamani Agosti 2, mwaka huu ambapo yalikuwa yanahakikiwa hadi juzi yalipokamilika kuhakikiwa na kufunguliwa na kupewa maombi namba 18 ya mwaka 2019.

 “Kwenye maombi yake, (Lissu) ameeleza sababu ya kuomba  amri ya mahakama kutengua tangazo  la kumvua ubunge na kiti chake kuwa wazi, ni kwamba uamuzi ulifanywa na Spika bila kuzingatia haki ya asili, bila ya kumsikiliza kwanza,” alidai Mughwai.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles