Derick Milton, Simiyu
Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), imesema itaendelea kuwa mdhamini mkuu wa maonyesho ya sikuu ya wakulima (Nanenane) kitaifa kwa mwaka 2020, ambayo yatafanyika tena katika Mkoa wa Simiyu.
Hayo yamesemwa na Meneja Mwandamizi wa Mahusiano na serikali wa benki hiyo William Kallaghe, wakati akionge na waandishi wa habari kwenye banda la benki hiyo wakati wa maonyesho hayo kitaifa 2019, yanayofikia kilele leo uwanja wa Nyakabindi mkoani Simiyu.
Kallaghe amesema kuwa benki hiyo inafanya hivyo ili kuweza kuwa karibu na wakulima, wajasiriamali na wafanyabishara mbalimbali katika kuhakikisha inawasaidia kwenye nyanja za mikopo na elimu katika kazi zao.
“Udhamini wa maonyesho haya mwaka 2020 utakuwa wa mara ya tatu mfululizo toka mwaka 2018, tutaendelea kuwa wadhamini wakuu katika kutimiza ahadi yetu kwa serikali ambayo tulisema tutadhamini kwa miaka mitatu,” amesema Kallaghe.
Amesema kuwa NBC imelenga kuhakikisha inawasaidia wakulima, wafanyabishara wa chini na kati ili waweze kuwa imara na kuchangia katika pato la taifa kupitia kulipa kodi ili Tanzania iweze kufikia uchumi wa kati 2025.