29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

Lugola ataka Magereza ijitosheleza kwa chakula

Mwandishi Wetu -Dodoma

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amepokea taarifa ya Bodi ya Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Magereza na kuwataka wajumbe wake kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha Magereza inajitosheleza kwa chakula.

Aliizindua bodi hiyo na kutoa miezi miwili wajumbe kutembelea miradi mbalimbali ya jeshi hilo na kumletea taarifa ya awali kuhusu miradi na maoni yao.

Akizungumza na baada ya kupokea taarifa yao Dodoma jana,  Lugola alisema taarifa waliyoiwasilisha ameifurahia, licha ya kuwa na upungufu ambao unahitaji uboreshaji zaidi.

Alisema bodi  ina wataalamu mbalimbali ambao wanaweza wakaleta mabadiliko makubwa ya uzalishaji mali na kuweza kufanikisha jeshi hilo kujitosheleza kwa chakula kupitia wafungwa mbalimbali waliopo magerezani.

“Nawapongeza kwa kazi nzuri, ila nawataka mfanye kazi zaidi ambayo itatuwezesha kuona mipango mizuri zaidi katika kulisimamia shirika hili ambalo bodi yake tuliizindua,” alisema Lugola.

Aliwataka Magereza kutumia wataalamu kupima viwanja vyao ili kufanikisha maendeleo zaidi na si kushirikiana na kampuni binafsi.

Mwenyekiti wa bodi hiyo, Meja Jenerali mstaafu, Raphael Muhuga, alisema kwa muda wa miezi miwili walitembelea mradi wa ng’ombe wa nyama Mbigiri, mradi wa maziwa Kingolwira, mradi wa uhunzi, kilimo Idete, kilimo Kiberege na Isupilo.

 “Pia miradi mingine tuliyoitembelea ni mradi wa kilimo Ludewa, mifugo Kitai na Mkwaya.

Katibu Mkuu wa Wizara, Meja Jenerali Jacob Kingu, aliitaka bodi ifanye ukaguzi wa kina wa mali za shirika hilo ili taarifa hizo zije kiuhalisia zaidi na kuleta mikakati imara ya mafanikio. 

Baadhi ya maelekezo aliyoyatoa Lugola kwa bodi hiyo, baada ya kuizindua, aliitaka kutekeleza maelekezo ya Rais John Magufuli kuhusu suala la magereza kujitosheleza kwa chakula.

Pia aliielekeza  itembelee magereza yote yenye miradi ya shirika na ifanye mkakati wa kutafuta wawekezaji kama vile kwenye mabwawa ya ufugaji wa samaki, na pia itoe mawazo mapya kuondoa kufanya biashara kwa mazoea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles