ELIZABETH HOMBO Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM
RAIS Dk. John Magufuli amezitaka nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), kufanya biashara kwa pamoja badala ya kufikiria kununua bidhaa nje ya nchi hizo.
Vilevile amezitaka nchi hizo kuhakikisha zinaondoa vikwazo vyote vinavyochangia kurudisha nyuma maendeleo ya sekta ya viwanda ndani ya jumuiya hiyo.
Rais Magufuli aliyasema hayo jana wakati akizindua maonyesho ya bidhaa katika Wiki ya Viwanda kwa nchi 16 wanachama wa SADC, Dar es Salaam.
Akizugumza katika uzinduzi huo, Ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Rais Magufuli alitumia lugha ya Kiswahili kati ya lugha nne zinazotumika SADC.
Lugha nyingine ni Kiingereza, Kireno na Kifaransa.
Pamoja na mambo mengine, Rais Magufuli alisema nchi za SADC zinapaswa kuweka kipaumbele kwenye teknolojia ya viwanda ndani ya nchi zao kabla ya kwenda mbali na zitumie pia malighafi kutoka katika nchi zao.
“Tumekuwa waagizaji wa bidhaa kutoka nje, ambazo zimekuwa na gharama kubwa.
“Pia nchi za Afrika zimekuwa wazalishaji wa nguvu kazi, vijana wanaikimbia Afrika ili kwenda Ulaya na Marekani ili kufanya kazi huko, kwa hiyo tukizitumia fursa za ndani ya Afrika tutapiga hatua kubwa.
“Tununue malighafi ndani ya SADC, pia tunao vijana wengi wenye uwezo wa sayansi na teknolojia, wengi wanakwenda kununua teknolojia kwa gharama kubwa ilhali kuna vijana wenye vipaji ndani ya nchi hizi 16.
“Viwanda vidogo ndivyo hukua na kuwa vikubwa, kukiwa na mazingira wezeshi kukuza uchumi na viwanda, nishati ya umeme wa uhakika, usafiri tutafika tunapopatarajia.
“Mara nyingi wanunuzi wa bidhaa ghafi ndio waamuzi wa bei kwa sababu wasipozinunua, sisi hatuna pa kuzipeleka, mwenendo huu ndio uliwadidimiza wakulima wetu kutokana na kutotabirika kwa bei.
“Kwa upande mwingine, nchi zetu zimeendelea kuwa waagizaji wa bidhaa za viwandani kutoka nje na bidhaa hizo zinazotokana na malighafi zetu huuzwa kwa bei kubwa,” alisema Rais Magufuli.
Alizitaka nchi hizo kushughulikia vikwazo vyote vinavyojitokeza, ikiwemo tozo mbalimbali na vikwazo vya mipakani ili kuwezesha viwanda na biashara.
Mbali na hayo, Rais Magufuli alieleza mambo yanayochagiza kukuza uchumi wa nchi za Afrika kupitia ushirikiano wa nchi hizo za SADC.
Katika hilo, alieleza masikitiko yake kuhusu mchango mdogo wa biashara zinazofanyika ndani ya bara la Afrika, huku sehemu kubwa ya bidhaa zinazouzwa nje ya bara hilo zikiwa ghafi.
“Licha ya umuhimu wa viwanda katika maendeleo ya nchi zetu, mchango wa sekta ya viwanda katika nchi nyingi za Afrika na za SADC bado ni mdogo sana, sekta hii inachangia wastani wa asilimia 10 tu ya pato la taifa na katika jumuiya yetu.
“Kwa sasa mchango wa bidhaa za viwandani za Afrika duniani ni chini ya asilimia tatu na hii ni kwa mujibu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, ingawa katika miaka ya karibuni kumekuwa na msukumo wa kukuza sekta ya viwandani barani Afrika.
“Kinachoshangaza zaidi ni namna wanunuzi wanavyotumia soko la Afrika, ambapo asilimia 62 ya bidhaa zinazouzwa nje ya bara hilo ni ghafi huku nchi za Afrika zikijiwekea vikwazo katika biashara za ndani,” alisema.
Alisema Afrika imechelewa kimaendeleo, hivyo nchi wanachama wa SADC hazina budi kuanza kukimbia kwa vitendo.
“Kukosekana kwa viwanda kunaifanya Afrika iendelee kuwa na uchumi tegemezi na hivyo kuendelea kubaki ndani ya mduara wa umasikini, hii ndiyo gharama ya kutokuwa na viwanda na hapa nimetoa mifano michache kuwaonyesha kwamba mapinduzi ya viwanda ni njia ya lazima kupitia kuelekea ukombozi wa kweli kiuchumi.
“Inaifanya Afrika kubakia tegemezi, hii ndiyo gharama ya kutokuwa na viwanda, mapinduzi ya viwanda ndiyo njia ya lazima kuelekea mapinduzi ya kiuchumi,” alisema Rais Magufuli.
Alisema nchi za SADC zinatakiwa kuwekeza katika viwanda vidogo ili kukuza uchumi na kupunguza umasikini wa watu wake, kuondoa vikwazo vya kibiashara na kuimarisha miundombinu inayounganisha nchi hizo.
“Tushughulikie vikwazo ndani ya SADC, tunawekeana vikwazo ambavyo havina maana yoyote, kuna utitiri mwingi wa kodi, hivi vyote tuviondoe.
“Tuwekeze katika mazingira wezeshi, ikiwamo umeme wa bei nafuu na uhakika, Tanzania tumeanza kuwekeza katika umeme wa Mto Rufiji, ujenzi wa SGR baadaye utaunganishwa hadi Uganda, tunajenga bandari.
“Pia tuhimize sekta binafsi katika kujenga viwanda, tuhimize, sekta binafsi ziache kulalamika, wanatakiwa kupigana na changamoto, hakuna cha bure bure.
“Ndani ya SADC kuna fursa nyingi, madini kila mahali, kuna madini, kilimo, uvuvi na kadhalika, soko letu ni kubwa, zaidi ya watu milioni 350, tuzichangamkie.
“Kutokana na kutokuwa na viwanda, urari wa biashara kati ya Afrika na mabara mengine umekuwa si mzuri. Mfano mwaka 2017 ambapo thamani ya biashara kati ya Afrika na Umoja wa Ulaya ilikuwa ni Sh trilioni 708 (Euro bilioni 280).
“Ambapo Afrika ilinunua bidhaa za Sh trilioni 376.7 (Euro bilioni 149) na ikauza bidhaa za Sh trilioni 331 (Euro bilioni 131), lakini asilimia 60 ya bidhaa ilizouza zilikuwa ghafi na hivyo kuwa na thamani ndogo,” alisema.
Rais Magufuli alisema ili kuepukana na upotevu wa fedha za kigeni, nchi za SADC zitekeleze kwa vitendo nguzo tatu za mkakati wa jumuiya hiyo wa maendeleo ya viwanda.
Alizitaja nguzo hilo ni kuhimiza maendeleo ya viwanda kama kichocheo cha mageuzi ya kiuchumi na kiteknolojia, kuongeza ushindani wa bidhaa za viwandani na kutumia mtangamano wa kikanda na jiografia yetu (yenye watu takribani milioni 350) kwa maendeleo ya viwanda na uchumi.
MAWAZIRI WA VIWANDA
Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa, alisema Tanzania imekuwa ikifanya vizuri katika biashara ndani ya SADC ambapo mauzo kwa mwaka jana yalikuwa Dola za Marekani milioni 999.34 ikilinganishwa na milioni 877.8 mwaka juzi.
Alisema pia uagizaji wa bidhaa toka SADC uliongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 600.64 hadi milioni 604.32 mwaka jana.
Kwa mujibu wa Bashungwa, bidhaa ambazo Tanzania inauza SADC ni madini mbalimbali kama vile Tanzanite na dhahabu, bidhaa za kilimo kama chai na kahawa, bidhaa za viwandani, plastiki, sigara na saruji, marumaru, madawa na vifaa tiba.
Alisema bidhaa ambazo Tanzania inanunua kutoka nchi za SADC zinahusisha magari, mbegu za mahindi, gesi, mabati, vilainishi, bia na sukari na zaidi zinatoka Afrika Kusini, Zambia, Mauritius na Malawi.
Bashungwa alisema maonyesho ya mwaka huu yanashirikisha washiriki 3,001 na kati yao waonyeshaji ni 1,576 ambapo Watanzania ni 1,404 na kutoka nje ni 172.
Waziri wa Viwanda na Biashara wa Zanzibar, Balozi Amina Ally, alisema udhaifu wa miundombinu na uhaba wa nishati ni moja ya changamoto inayozorotesha uendelezaji wa viwanda katika nchi nyingi.
“Uchumi wa viwanda unategemea sana kuimarika kwa sekta nyingine katika nchi kama nishati, hivyo ni muhimu nchi wanachama kutilia mkazo uimarishaji wa sekta nyingine,” alisema Balozi Amina.
KATIBU MTENDAJI SADC
Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya SADC, Dk. Stergomena Tax, alisema ushiriki wa Tanzania bado ni mdogo katika jumuiya, lakini fursa bado zipo nyingi.
Kwa mujibu wa Dk. Tax, idadi ya watu katika nchi za SADC ni milioni 344 na pato la taifa ni Dola za Marekani milioni 2.3.
“Kuna fursa kubwa ya soko la huduma kwa sababu vikao si chini ya 30 vitafanyika Tanzania, hivyo kuna haja ya kujadiliana namna gani fursa hizo zitumiwe,” alisema Dk. Tax.
Mwenyekiti wa Baraza la Biashara la SADC aliyemaliza muda wake, Charity Mwiya kutoka Namibia, alihimiza kuwapo kwa jitihada za pamoja baina ya sekta ya umma na binafsi ili kufikia malengo ya mkakati wa viwanda wa jumuiya hiyo.
“Kunatakiwa kuwepo na mazingira wezeshi kwa sekta binafsi ili iweze kutoa ajira kwa wingi, hasa kwa vijana,” alisema Mwiya.