MWANDISHI WETU
Wakala wa Dijitali na Teknolojia nchini Smart Codes, wamezindua upya bidhaa ya M-Paper kwenye kampeni iitwayo “Kurasa Zinaongea” ili kutanua wigo wa bidhaa za magazeti ambapo kwa sasa wateja watayapata kuanzia saa sita usiku kupitia simu za mikononi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Mkurugenzi Mtendaji wa Smart Code, Edwin Bruno alisema ujio mpya wa Mpaper utachangia kutanua wigo wa biashara ya magazeti kupitia digitali na kuongeza mapato kwa kampuni za uzalishaji wa magazeti hayo.
Alisema Mpaper inawezesha wasomaji kupata taarifa za magazeti yote zilizodhibitishwa ikiwamo kampuni zinazotafuta tenda au mtu yeyote anayetaka kupata habari za magazeti yote ya mahali popote na wakati wowote kuanzia usiku wa manane kwa simu ya mkononi au tovuti ya Mpaper.
“M-Paper sasa inasimama kama bidhaa huru ya kibiashara iliyochapishwa upya na huduma ambazo ni pamoja na njia ya kirafiki zaidi kwa watumiaji, usajili na kujiunga kwa namba ya simu, sehemu ya kuchati na upatikanaji wa masaa 24 kwa timu ya Mpaper, vifurushi vya malipo ya kirafiki, chaguzi za malipo zaidi kwa M-pesa, Tigo pesa, Airtel Money na kuunganishwa kwa mfumo wa benki ambayo inaruhusu jamii ya diaspora kulipa kupitia Visa au Kadi ya Master,” alisema.
Aidha, Meneja wa mradi wa Smart Codes, Reuben Orinda alisema kampeni ya “Kurasa Zinaongea” inaelezea wazo la kupata kurasa zote za magazeti kwa njia ya digitali kwa nusu bei ya gazeti husika.
Alisema kampeni hiyo itaendeshwa kwa miezi ijayo katika chaneli zote za mawasiliano na kurasa za kijamii za M-Paper ili kufundisha wateja wa sasa na wapya juu ya jinsi ya kupakua na kutumia M-Paper na pia kujenga mwamko wa huduma zilizoongezwa kama thamani ya kifungu cha malipo ya pesa, msaada wa huduma kwa wateja, na mengi zaidi.
Wakati Meneja wa biashara Sharron Nsule alisema moja ya changamoto inayokabili bidhaa za magazeti ni uchache wa bidhaa hiyo kutokidhi mahitaji ya wateja lakini sasa kupitia Mpaper itasaidia upatikanaji wa bidhaa hizo kwa urahisi.
“Kabla ya hapo kuna changamoto kwani awateja walikuwa wanapata baadhi ya magazeti, lakini Mpaper imeboreshwa na sasa unaweza kuyapata magazeti kuanzia saa sita usiku na habari zote zilizothibitishwa unaweza kuzipata kupitia kiganja chako kwa muda wote mahali popote kuanzia ukurasa wa kwanza mpaka wa mwisho.