Damian Masyenene, Mwanza
WAKATI dirisha la usajili kwa timu za Ligi Kuu, Daraja la Kwanza na la Pili Tanzania Bara limepangwa kufungwa leo, Klabu ya Alliance imeweka wazi majina ya wachezaji wake itakaowatumia msimu ujao.
Mbalia ya kuanika majina ya wachezaji itakaowatumia, pia klabu hiyo ya Mwanza imeanika orodha ya wachezaji ilioachana nao kutokana na sababu tofauti.
Katika orodha hiyo, Alliance imewasajili mshambuliaji mkongwe, Jerrison Tegete ambaye amewahi kutamba na Yanga, Majimaji na Kagera Sugar.Pia imemsajili
mchezaji wao wake wa zamani, Athanas Mdamu aliyekuwa akikipiga Kariobangi Sharks ya Kenya.
Wengine waliomwaga wino klabu hapo
ni Abdulkarim Hamim, Peter Mwangosi,
Erick Murilo, Hussein Kasanga( Mbao FC), Daniel Manyenye (Biashara United),
Selia Gambareko (Western Stima, Kenya), Sixtus Mwasekaga (Stand United) na
Deusdedith Okoyo aliyejiunga na timu hiyo akitokea
Geita Gold.
Mwenyekiti wa Mashindano Alliance, Yusuph Budodi alisema nyota wao 16 wa kikosi cha msimu uliopita wataendelea kuwa nao, huku tisa wakiondoka, ambapo wachezaji wapya 12 wamesajiliwa.
Aliwataja walioachana nao kuwa ni mlinda mlango, Ibrahim Isihaka, Dickson Ambundo, Bigirimana Blaise, Hussein Javu, Jamal Mtegeta, Rajabu Kibera,Mapinduzi Balama, Nteze John na Paul Mahona.
Akizungumzia maandalizi ya timu, Msemaji wa Alliance, Jackson Mwafulango alisema kikosi chao tayari kimeshaanza mazoezi na wameandaa utaratibu wa maandalizi, ambapo wanasubiri pendekezo la benchi la ufundi kuhusu wapi timu ifanyie maandalizi yake na mechi za kirafiki.
Mwafulango alisema nafasi mbili zilizobaki za usajili wanatarajia kuzijaza kwenye dirisha dogo.