NEW YORK, MAREKANI
RIPOTI mpya ya Umoja wa Mataifa (UN) imesema zaidi ya watoto 12,000 wameuawa na kujeruhiwa katika mizozo ya kivita mwaka jana, asilimia kubwa wakiwa ni kutoka Afghanistan, Palestina, Syria na Yemen.
Aidha ripoti hiyo ilisema vifo hivyo na majeraha ni miongoni mwa zaidi ya matukio 24,000 ya ukiukaji dhidi ya watoto yaliyothibitishwa na UN ikiwa ni pamoja na kutumikishwa jeshini kama wapiganaji, dhuluma za kingono, utekaji na mashambulizi shuleni na hospitalini.
Ripoti ya kila mwaka ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres kwa Baraza la Usalama kuhusu watoto katika mizozo ya vita, inasema ukiukaji unaofanywa na makundi ya wapiganaji upo pale pale, lakini kuna ongezeko la matukio ya ukiukaji unaofanywa na wanajeshi wa Serikali na kimataifa ikilinganishwa na mwaka juzi.
Orodha inayosubiriwa kwa hamu kutolewa na Guterres ya nchi ambazo zimefanya ukiukaji mkubwa wa haki za watoto wakati wa migogoro, inaonekana kutokuwa na tofauti kubwa na ya mwaka jana, kitu kinachoyakasirisha makundi ya haki za binadamu.
Mashirika ya Human Rights Watch na Watch list on Children Armed Conflict, yamekasirishwa na kubakishwa muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia kwenye orodha ya wahusika ambao wameweka hatua za kuwalinda watoto, yakitaja ongezeko la vifo vya watoto vinavyosababishwa na wanajeshi wa Serikali na wa muungano nchini Yemen.
Afghanistan inaongoza orodha hiyo ambapo watoto 3,062 waliripotiwa kuuawa mwaka jana, nchini Syria mashambulizi ya angani, mabomu ya mapipa na ya kutapakaa yaliwaua na kuwajeruhi vijana 1,854 na nchini Yemen, watoto 1,689 waliuawa kutokana na mapigano.
Katika mzozo wa Israel na Wapalestina, Umoja wa Mataifa umesema watoto wengi waliuliwa mwaka jana huku kukiwa na idadi iliyothibitishwa ya watoto 59 wa Kipalestina na 2,756 kujeruhiwa.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, pande zinazohasimiana Somalia ziliwaingiza jeshini na kuwatumikisha watoto 2,300, wengine wakiwa na umri mdogo kabisa wa miaka nane. Wanamgambo wa Al-Shabaab waliongeza kwa kiasi kikubwa usajili wao kwa kuwaingiza jeshini vijana 1,865.
Nigeria ilikuwa katika nafasi ya pili, ambapo watoto 1,947 waliingizwa vitani, wakiwemo baadhi waliotumiwa kama walipuaji wa kujitoa mhanga.
Somalia pia ilikuwa na idadi kubwa ya takwimu zilizothibitishwa za unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto, ambapo visa 331 viliripotiwa mwaka jana, ikifuatwa na Congo na visa 277 ijapokuwa Guterres anasema matukio bado hayaripotiwi sana, hasa kuwahusu wavulana kwa sababu ya unyanyapaa.
Somalia pia ilikuwa na idadi kubwa ya watoto waliotekwa nyara mwaka jana ambao ni 1,609.
Guterres alisema maelfu ya watoto pia waliathiriwa na mashambulizi 1,023 yaliyothibitishwa kufanywa kwenye shule na hospitali mwaka jana.
Nchini Syria, kulikuwa na mashambulizi 225 kwenye shule na vituo vya afya mwaka jana, ikiwa ndiyo idadi kubwa tangu kuanza kwa vita mwaka 2011.
Aidha kumekuwa na ongezeko la mashambulizi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, Colombia, Libya, Mali, Nigeria, Somalia, Sudan na Yemen.