Safina Sarwatt -Rombo
WAKULIMA wa ndizi Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, wameomba Wizara ya Kilimo kuwapatia pembejeo ili kuongeza tija kwenye uzalishaji wa zao hilo.
Wakulima hao, walisema kuwa kilimo cha ndizi kina soko kubwa kuliko kahawa na kwamba changamoto kubwa ni upatikanaji wa mbegu bora za migomba.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wilayani hapo jana, walisema wanashindwa kuzalisha ndizi zenye ubora, licha ya kuwapo soko la uhakia.
Ansila Lyimo, alisema uzalishaji wa zao hilo ni mdogo kutokana na wengi wao kuzalisha ndizi kwa chakula na si biashara, licha ya zao hilo kwa sasa kuonekana kufanya vizuri baada ya kilimo cha kahawa kukosa soko.
Mtaalamu wa kilimo kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari), Juma Kitundu, alisema Serikali imeanza mpango wa kuwezesha wakulima wa ndizi kuboresha kilimo ili kuongeza uzalishaji wa ndizi bora zitakazokidhi soko la ndani na nje ya nchi.
Akizungumza na wakulima hao, Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Agness Hokororo, alisema sasa zao hilo ndilo la kibiashara baada ya mazao mengine kukosa masoko ya uhakika.