Theresia Gasper -Dar es salaam
MASHABIKI na wanachama wa Yanga wameendelea kujitokeza kwa wingi katika Wiki ya Wananchi, huku wakifanya shughuli mbali mbali za kijamii.
Wiki ya Wananchi ilianza tangu wiki iliyopita katika mikoa mbalimbali nchini huku wakionekana kuitikia wito kwa wingi.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Katibu Mkuu wa kamati ya hamasa, Deo Mutta, alisema mashabiki na wanachama wameendelea kujitokeza kwa wingi baada ya kuhamasika.
“Leo (jana) tupo Bagamoyo ambako tuna tamasha la funga kijiji na baadaye kesho tutaenda Kibaha na Mlandizi na tutamalizia Morogoro kabla ya kurejea tena Dar es Salaam,” alisema.
Mutta alisema timu ya Yanga inatarajia kurudi Dar es Salaam kesho ambapo itasindikizwa na mashabiki kutoka Morogoro hadi jijini hapa.
Alisema wataendelea na shughuli mbalimbali ikiwemo kufanya usafi hospitalini hadi kilele cha tamasha hilo ambalo litakua mechi ya kirafiki kati ya Yanga na Kariobangi Sharks ya Kenya Agosti 4, mwaka huu katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mchezo huo ni maandalizi ya mechi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Township Rollers ya Botswana unaotarajiwa kuchezwa kati ya Agosti 9 na 11 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kurudiana kati ya Agosti 23 na 25 mwaka huu nchini Botswana.