26.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 25, 2024

Contact us: [email protected]

Baba, mtoto mbaroni kwa tuhuma za hongo

Ramadhan Hassan -Dodoma

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAkukuru),  Mkoa wa Dodoma inawashikilia wafanyabiashara ambao ni baba na mwanawe kwa tuhuma za kumpa rushwa ya Sh milioni 1.2  Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi.

Watuhumiwa hao walitarajiwa kupandishwa kizimbani jana kujibu tuhuma hizo katika Mahakama ya Wilaya ya Dodoma Mjini.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Dodoma, Sostenes Kibwengo, alisema wanawashikilia wanaume wawili ambao ni Bahadur Abdalah Hirji (68), mfanyabiashara na mkazi wa Mtaa wa Tembo, Kata ya Madukani Dodoma na mwanawe Nahid Bahadur Hirji (33) ambaye ni Mhasibu wa Kampuni ya Victory Bookshop Ltd ya jijini hapa.

Kibwengo alisema kosa la watuhumiwa hao ni kuahidi na kutoa hongo ya Sh milioni 1.2  kwa Katambi ili asifuatilie mapungufu katika ombi la utekelezaji wa amri ya Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Dodoma ya kukazia hukumu lililowasilishwa kwake na dada wa Bahadur Hirji.

“Baada ya kupata taarifa ya watuhumiwa kuahidi kutoa fedha hiyo kama kishawishi kwa Mkuu wa Wilaya, tulianza kuwafuatilia na kufanikiwa kuwakamata tarehe 27 Julai, 2019 majira ya saa 11 jioni katika Hoteli ya Royal Village, Area D jijini Dodoma mara baada ya mtuhumiwa Nahid kumkabidhi Mkuu wa Wilaya rushwa hiyo,” alisema Kibwengo.

Katika hatua nyingine, Takukuru Mkoa wa Dodoma pia inamshikilia Omary Mtauka ambaye ni msaidizi wa Mtendaji wa Kata ya Makutupora, ambaye anadaiwa kuomba na kupokea hongo ya Sh 110,000 kutoka kwa mzee mwenye umri wa miaka 78, Paulo Mawope, mkazi wa Chilungule Kata ya Makutupora.

“Alichukua ili amalize tuhuma dhidi yake za kugombana na jirani zilizowasilishwa kwa Mtendaji wa Mtaa na baadaye ofisi ya kata.

“Awali, tulipokea taarifa kutoka kwa mjukuu wa mzee huyo kwamba alipigiwa simu na Mtendaji wa Kata ya Makutupora akitakiwa kutoa fedha hizo ili babu yake aliyekuwa ameshtakiwa katika ofisi ya kata aachiwe.

 “Baada ya kumkamata, tulibaini mtuhumiwa ni msaidizi wa Mtendaji wa Kata ya Makutupora na alikamilisha uhalifu wake kwa kujifanya ni Mtendaji wa Kata,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles