29.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 1, 2023

Contact us: [email protected]

Madiwani wavua majoho kikaoni, wamkataa DED

Kadama Malunde -Shinyanga

MADIWANI wa Manispaa ya Shinyanga wakiongozwa na wa CCM, wamemkataa Mkurugenzi Mtendaji wa manispaa hiyo, Geofrey Mwangulubi kwa madai ya kushindwa kutekeleza maagizo mbalimbali yanayotolewa kila mara katika vikao vya baraza.

Wamedai tabia ya mkurugenzi huyo kushindwa kutekeleza maagizo wanayoyatoa katika vikao, huenda ikawachonganisha na wapigakura wao kutokana na kutokuwepo kwa miradi yoyote ya maendeleo inayotekelezwa katika kata zao.

Hali hiyo imejitokeza jana katika kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani wakati madiwani hao wakiidhinisha ajenda zilizopangwa kujadiliwa.

Diwani wa Kata ya Ndembezi, David Nkulila (CCM),  alisimama na kuzikataa ajenda hizo na kisha kutoa hoja yake ya kutokuwa na imani na Mkurugenzi Mwangulumbi.

Hoja ya Diwani Nkulila, iliungwa mkono na baadhi ya madiwani ambapo hata hivyo, Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Shinyanga (Serikali za Mitaa), Alphonce Kasanyi, na mwanasheria wa manispaa hiyo, Doris Dario walisimama na kuwataka madiwani kusitisha uamuzi wao kwa vile unapingana na utaratibu.

Kasanyi alisema madiwani walipaswa waitishe kikao maalumu cha kutokuwa na imani na mkurugenzi pamoja na kumwandikia barua mkuu wa mkoa kuhusu kumkataa mkurugenzi huyo.

Hata hivyo, ushauri wa Katibu Tawala Msaidizi na mwanasheria wa Manispaa ya Shinyanga, uligonga mwamba baada ya baadhi ya madiwani kusimama na kuanza kuchambua hoja hiyo ikiwamo maagizo yaliyotolewa kwenye vikao vya Baraza la Madiwani jambo walilodai ni dharau inayooneshwa kwao na hawako tayari kufanya naye kazi.

Diwani wa Viti Maalumu, Shella Mshendate (CCM), alisema hawako tayari kuendelea kufanya kazi na Mwangulumbi na kitendo chao hakimaanishi kuvunja baraza bali hawamtaki mtu.

Alimwomba Naibu Meya atafute mtaalamu mwingine akae kwenye kiti cha mkurugenzi na kikao kiendelee.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Mwangulumbi, alisema hawezi kuzungumza chochote kuhusu uamuzi wa madiwani hao, anasubiri uamuzi kutoka ngazi za juu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,404FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles