NEWYORK, MAREKANI
SHIRIKA la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya nishati ya nyuklia limetangaza kuwa litakutana kesho kuanza mchakato wa kumtafuta mkurugenzi mkuu atakayeichukua nafasi ya Yukiya Amano aliyefariki dunia wiki iliyopita.
Wadhfa huo katika shirika la IAEA ni muhimu sana hasa ukizingatia wasiwasi unaoongezeka kuhusiana na shughuli za nyuklia za Iran.
Miongoni mwa wale wanaotajwa kuwa na uwezekano wa kuichukua nafasi ya Amano ni Cornel Feruta wa Romania, aliyekuwa mshirika wake wa karibu na ambaye kwa sasa ni mratibu mkuu wa shirika hilo.
Mwingine ni Rafael Grossi, balozi wa Argentina katika shirika hilo la Umoja wa Mataifa. IAEA ilisema jana kuwa mkutano huo maalum wa bodi ya magavana utamchagua pia kiongozi wa mpito kutokana na mchakato wa kumpata kiongozi wa kudumu kuchukua muda mrefu.