25.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

JPM kuweka jiwe la msingi mradi wa Stiegler’s Gorge

Bakari Kimwanga-Morogoro

RAIS Dk. John Magufuli kesho anatarajiwa kuweka jiwe la msingi mradi wa kuzalisha umeme wa maji maporomoko ya Mto Rufiji (Stiegler’s Gorge) ambao ujenzi wake utakamilika ndani ya miezi 35.

Mradi huo ambao ujenzi wake umefika asilimia 15, hadi kukamilika utagharimu Sh trilioni 6.5.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mradi huo mjini Morogoro jana, Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, alisema kukamilika kwake kutaweka historia nyingine kwa nchi na usimamizi unaofanywa na Rais Dk. Magufuli.

Alisema mradi huo wa kufua umeme wa megawati 2,115 kwa kutumia maji, unaendelea kutekelezwa na sasa uko tayari kuwekwa jiwe la msingi.

“Kwa hatua za usimamizi wa mradi hadi sasa tupo asilimia 100, ila katika hatua za utekelezaji wake tupo asilimia 15 hadi sasa.

“Mkandarasi alikuwa na kazi ya kukabidhiwa maandalizi ya mradi na kazi ambayo anaendelea nayo ni kuchoronga eneo la bwawa na ujenzi wa madaraja.

“Kukamilika kwa mradi kutaliwezesha taifa kuwa na umeme wa kutosha na wa uhakika, unaotabirika na wa gharama nafuu kwa watumiaji,” alisema Dk. Kalemani.

Alisema mradi huo utawezesha nchi kufikia uchumi wa viwanda na kuimarisha shughuli za kiuchumi na kijamii kwa kuendeleza kilimo cha umwagiliaji, uvuvi, kukuza utalii na kuongeza ajira kwa Watanzania.

MANUFAA

Dk. Kalemani alisema hadi sasa mradi umetoa ajira 600 za kudumu  kwa Watanzania ingawa hadi kukamilika kwake utakuwa na ajira 6,000 ikiwamo kazi za vibarua.

Alisema hadi sasa vijiji 22 ambavyo vipo jirani na eneo la mradi, vimeunganishwa na huduna ya umeme kwa gharama ya Sh 27,000 na mradi utakapokamilika, vijiji vingine 37 vitaunganishiwa umeme.

“Mradi huu utakuwa na manufaa kwa nchi kwani utaokoa misitu mingi ambayo imekuwa ikikatwa kwa ajili ya mkaa.

“Leo Dar es Salaam pekee inatumia magunia 500,000 kwa siku na misitu ekari nne imekatwa, hasa katika mikoa ya Pwani, Morogoro na Iringa.

“Hadi kufikia 2030 ekari milioni 2.8 zingekatwa kwa ajili ya nishati ya mkaa, lakini mradi huu wa kufua umeme katika maporomoko ya maji Mto Rufiji unakuja kuokoa taifa letu,” alisema Dk. Kalemani.

Akizungumzia faida za utalii, alisema hadi kukamilika kwa bwawa hilo ambalo ni la 70 duniani na la 60 kwa Afrika, litachochea shughuli za utalii eneo hilo la mradi katika Pori la Akiba la Selous.

“Wizara ya Nishati inapenda kuwahakikishia  Watanzania kuwa tutatekeleza wajibu wetu kwa kasi, weledi na nidhamu katika kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli katika kuleta maendeleo ya nchi yetu na kujenga Tanzania kwa kutambua kwamba nishati ndiyo injini katika kujenga uchumi wa viwanda.

“Ninawakaribisha wananchi wote waliopo vijiji vyote vya jirani na eneo la mradi kuhudhuria keshokutwa (kesho) katika uzinduzi huu wa uwekaji jiwe la msingi ambao utafanywa na Rais Dk. Magufuli,” alisema Dk. Kalemani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles