28.3 C
Dar es Salaam
Monday, July 22, 2024

Contact us: [email protected]

Mangula atoa onyo wanaojipenyeza kuwania ubunge

MWANDISHI WETU-SINGIDA

MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Philip Mangula, ameonya wanachama wa chama hicho wanaojipenyeza kuwania ubunge na udiwani wakati viti hivyo bado vina watu.

Alitoa onyo hilo Wilaya ya Ikungi mkoani Singida wakati wa mkutano kuwapongeza wanaCCM wa Jimbo la Singida Mashariki kbaada ya Miraji Mtaturu kutangazwa kuwa mbunge akimrithi Tundu Lissu.

“Natoa maelekezo kuwa mtu yeyote atakayebainika kuanza kujipenyeza kwenye majimbo kuanza kufanya kampeni ya kuwania nafasi hizo za uongozi hatutamwonea huruma, tunamchukulia hatua za kinidhamu,” alisema Mangula.

Alisema katika majimbo kuna wawakilishi ambao muda wao wa miaka mitano bado haujaisha, hivyo waachwe watekeleze ilani ya chama hicho kwa kuwapelekea wananchi maendeleo.

Alisema mwanaCCM mwenye nia ya kutaka nafasi hizo, anatakiwa kusubiri muda utakapofika na wanachotakiwa sasa ni kwenda kwa wananchi kutangaza kazi za maendeleo zilizofanywa na viongozi waliopo madarakani.

Alitoa maagizo kwa wanaCCM kuwa pindi watakapomwona mtu yeyote ameanza kujipenyeza katika majimbo hayo, watoe taarifa ili aweze kuchukuliwa hatua kupitia kamati ya maadili.

Mangula ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya chama hicho, alielezea umuhimu wa kutoa elimu ya mpigakura ili kila mtu aweze kujua haki yake ya kupiga kura.

Alisema katika uchaguzi mkuu uliopita katika baadhi ya maeneo, watu waliojitokeza kupiga kura walikuwa wachache kutokana na kutokuwepo elimu hiyo.

Mangula alisema hali hiyo ilifanya kiongozi achaguliwe kwa kura chache, akitolea mfano Jimbo la Igalula mkoani Tabora ambako idadi ya wapigakura walikuwa ni asilimia 22 pekee.

“Kuna umuhimu mkubwa wa kutoa elimu hii walau mgombea aweze  kupata zaidi ya asilimia 40 kuliko kuwa chini ya hapo,” alisema Mangula.

Alisema mapambio, chereko chereko na watu wengi katika mikutano ya kampeni hayawezi kuongeza idadi ya wapigakura kama hakuna elimu hiyo.

Mangula alitumia hafla hiyo kumkabidhi Mtaturu ilani ya uchaguzi ya chama hicho ya mwaka 2015/20 ikiwa ni ishara ya kuanza kazi ya kuwatumikia wananchi wa Singida Mashariki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles