33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Bashe: Tuna chakula cha kutosha kuisaidia Kenya

ANDREW MSECHU – dar es salaam

NAIBU Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, amesema Tanzania iko tayari kutoa chakula kusaidia Kenya kwa kuwa ina hifadhi ya kutosha ya chakula.

Akizungumza Ikulu Dar es Salaam jana, Bashe alisema kwa sasa kutokana na uhaba wa chakula unaoendelea Kenya, Tanzania itatumia nafasi yake ya ujirani mwema kutoa chakula, hasa mahindi na unga, kwa makubaliano rasmi yatakayofikiwa baina ya pande hizo mbili.

Alisema Bodi ya Mazao inayoongozwa na Monica Mbega ina hifadhi kubwa ya mahindi ambayo imekuwa ikiyatafutia masoko nje.

 “Niwahakikishie ndugu zetu wa Kenya kuwa udugu ni kufaana, kwa hiyo sisi kama ndugu, hii pia ni fursa ya kibiashara na tutafaana katika hili,” alisema.

Bashe alisema kuna vinu viwili ambavyo Serikali inavisimamia na vinahitaji kufanya kazi, hivyo wizara yake ipo tayari kuvitoa kutumiwa na wafanyabiashara wa Kenya watakaonunua mahindi na kutaka kuyasaga.

Alisema wafanyabiashara wa nchi hiyo wenye kuhitaji mahindi wawasiliane na wizara hiyo ili kuwasaidia wafanikishe azma yao hiyo bila ukiritimba wa aina yoyote.

UJUMBE WA KENYA

Kauli ya Bashe ilikuja baada ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo ya Kenya, Profesa Fred Segor, kusema mwaka huu wana changamoto ya hali ya hewa, kwa kuwa mvua imekataa hadi magazeti yakaandika ‘mvua iliyotakiwa kunyesha Kenya imekwama Tanzania’.

“Mwezi wa nne mvua ilikuja kwa kuchelewa na iliisha mapema, kwa hiyo kutakuwa na upungufu wa mahindi. Kwa takwimu tunaona tutapata asilimia 60 ya mahitaji yetu ya kawaida,” alisema.

Profesa Segor alisema kwa mwezi mmoja Wakenya wanatumia magunia milioni nne ya mahindi kwa matumizi mbalimbali, ambayo yanayosagwa kwa ugali ni milioni 1.5 na wengine wanatumia kupika makande  shuleni.

Alisema kwa sababu hiyo, wanaomba wachanganyiwe unga na mahindi ili shule zisitaabike, lakini pia kuna sehemu nyingine kame zaidi kama Turkana ambazo inabidi wapeleke vyakula.

“Tunaona tutakuwa na changamoto hii kuanzia katikati ya Agosti hadi mwishoni mwa Oktoba au Novemba, lakini pia Aprili na Mei kutakuwa na kiangazi ambapo bei za vyakula zinafumuka na kuwa juu,” alisema.

Alisema duniani Kenya ni nchi ya pili kwa gharama za juu kwenye chakula na Mkenya wa kawaida anatumia asilimia 50 ya fedha zake kununua chakula.

Awali, Rais John Magufuli alisema katika mazungumzo yake na Rais Uhuru Kenyatta alipomtembelea nyumbani kwake Chato, alizungumzia ununuzi wa mahindi kutoka Tanzania, ambapo alizungumza na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi kuhusu namna viwanda vya kuchakata nafaka vya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) vitakavyoweza kutumika.

Rais Magufuli alisema suala muhimu kwa sasa ni kwa wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo kukaa na kukubaliana na wale wa JKT namna watakavyoweza kutumia fursa hiyo kununua mahindi kwa wakulima, kuyasaga na kuyauza yakiwa tayari yameshaongezwa thamani.

Alisema katika hilo, si fursa kwa viwanda vinavyomilikiwa na vyombo vya usalama tu, bali pia wafanyabiashara binafsi wanaruhusiwa kufanya kazi hiyo kwa makubaliano maalumu.

MAHITAJI YA GESI

Rais Magufuli alisema pamoja na mambo mengine, Rais Kenyatta alieleza makusudi yake ya kununua gesi kutoka Tanzania na sasa ameamua kutuma ujumbe wake kutekeleza makubaliano rasmi.

Akizungumzia suala hilo, mjumbe mwingine kutoka Kenya, alisema awali walitaka kununua gesi Qatar, lakini baadaye wakaona hakuna haja ya kufanya hivyo kwakuwa nishati hiyo ipo Tanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles