NA ALLAN VICENT, TABORA
NAIBU Waziri wa Nishati, Subira Mgallu amewataka wana vijiji zaidi ya 400 katika vijiji vitatu waliopata umeme wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA) Kata ya Kitunda wilayani Sikonge kutofurahia umeme, bali wautumie kama fursa ya kuwekeza ili kukuza uchumi wao.
Alitoa kauli hiyo juzi, alipokagua mradi wa umeme wa jua uliokamilishwa vijiji vya Mgambo, Mwenge na Mkola.
Alisema umeme, ni fursa muhimu ya kusukuma maendeleo ya mtu mmoja mmoja, kijiji, kata, tarafa, wilaya, mkoa na taifa kwa ujumla katika nyanja zote.
Alisema Serikali kupitia mradi wa PowerCornar, imedhamiria kuhakikisha vijiji vyotevilivyokuwa na adha ya ukosefu wa nishati hiyo kwa muda mrefu, vinapata.
Alisema mkakati wa Serikali, ni kuhakikisha huduma hiyo inapelekwa maeneo yote yasiyofikika ili wananchi waweze kufaidi matunda ya uhuru wa nchi yao.
Alisema ili kufanikisha mpango huo, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na REA, walitafuta kampuni hiyo ili ƙufanikisha mkakati huo na wananchi wanalipia gharama kidogo tu ya sh 27,000/-.
Meneja Mkuu wa Kanda ya Magharibi wa Kampuni ya PowerCornar, Mhandisi Erick France alisema hadi sasa kazi imetekelezwa kwa asilimia 100 katika vijji hivyo.
Alisema waliounganishiwa umeme hadi sasa kwa kijiji cha Mgambo, ni wateja 174 na vijiji vya Mwenge na Mkola ni wateja 321.
Alisema hadi sasa, wamezalisha kilowati 20 kwa kijiji cha Mgambo na umeme wa kilowati 28 kwa vijiji vya Mwenge na Mkola.