MWANDISHI wetu-MOROGORO
KATIBU wa CCM Mkoa wa Morogoro, Shaka Hamdu Shaka, amesema chama hicho kimepita katika mawimbi makubwa kuliko sasa ambapo kipo kwenye mikono salama ya Mwenyekiti wake Rais Dk. John Magufuli.
Amesema kiongozi huyo ni nahodha mzuri mwenye kujua uwezo wa chombo ambacho kwa sasa kipo katika mikono salama baharini na nchi kavu.
Hayo aliyasema juzi mjini hapa, alipokuwa akizungumza na wanachama wa CCM katika Kata ya Mafisa.
Alisema kuwa Rais Magufuli ni kiongozi mwenye kuhimili kila aina ya mikiki, na bado chombo kimebaki imara.
“CCM imepitia katika nyakati ngumu sana na imeendelea kuwa imara siku hadi siku, nahodha wetu ndani ya chombo, usukani ameudhibiti vyema, anahimili na kupambana na mawimbi makubwa yanayoambatana na pepo za kusi na kasi, mabaharia wote wako makini na abiria wametulia.
“Jahazi la CCM halijawahi kukabidhiwa mtu dhaifu wala legelege, nawahakikishia tutavuka salama na tutaendelea kuwa wamoja wenye upendo na mshikamano chini ya Mwenyekiti Dk. Magufuli,” alisema Shaka.
Alisema kitendo chochote cha kumbughudhi mwenyekiti wao Rais Magufuli katika kipindi chake cha uongozi wa miaka 10 hali ya kuwa hakijamalizika, hakiwezi kuvumiliwa kwani anayewaza kutenda jambo hilo atahesabiwa kama baharia mdandia meli asiye na cheti cha kazi hiyo.
Shaka alisema CCM ndiyo iliyompa dhamana na amana mwanachama wake kwa miaka 10, haiwezekani kumwambia akae pembeni ili apishe mtu mwingine wakati bado hajamaliza muda wake wa uongozi.
“Viongozi wa CCM ngazi zote chapeni kazi, timizeni wajibu wenu wa kikatiba na kikanuni. Chama chetu ni kikubwa na imara mno, kina viongozi wazoefu, walio na busara na hekima.
“Wapinzani ni mapoyoyo, wanapenda upekepeke, udaku na ushabiki, usiku na mchana wanaomba CCM igawanyike, hilo katu halitatokea, CCM ina mbavu za kuhimili aina ya misukosuko na dhoruba hatimaye kikavuka kikiwa salama.
“Watanzania tuendelee kusimama pamoja na Rais Magufuli wakati wote kwakuwa ni kiongozi aliyeamua kwa dhati kuwatumikia wananchi, akijali dhiki na shida na kutaka kuwafikisha kwenye nchi ya neema na ustawi,” alisema Shaka.