26.8 C
Dar es Salaam
Saturday, September 7, 2024

Contact us: [email protected]

Ummy aeleza upatikanaji dawa ulivyoimarika

ANDREW MSECHU-DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amesema Serikali imeimarisha upatikanaji wa dawa katika hospitali zake hadi kufikia zaidi ya asilimia 90 kwa sasa.

Akizungumza katika mkutano baina ya Bohari Kuu ya Dawa (MSD) na wazalishaji na wasambazaji wa dawa nchini mwishoni mwa wiki, Ummy alisema bado Serikali inaimarisha upatikanaji wa dawa katika hospitali zake ili kuhakikisha tatizo la dawa linakuwa historia.

“Tunatarajia kuimarisha zaidi upatikanaji wa dawa katika hospitali zetu. Moja ya mikakati tuliyonayo ni kuhakikisha tunanunua dawa na vifaa tiba kutoka kwa mawakala wa uzalishaji wa ndani, hatua ambayo inasaidia kupunguza gharama,” alisema.

Ummy alisema katika utaratibu huo, wameweza kupunguza gharama, akitolea mfano ununuzi wa mashuka ya wagonjwa, ambapo awali walikuwa wakinunua shuka moja kwa Sh 21,000 lakini baada ya kuingia mkataba wa muda mrefu na wazalishaji, walipunguza gharama hadi Sh 12,000.

Aliwataka watu wenye uwezo wa kuwekeza katika uzalishaji wa dawa na vifaa tiba kujitokeza kwa wingi kwa kuwa kwa sasa ni asilimia sita tu inayonunuliwa kutoka ndani ya nchi, hivyo kufanya fedha nyingi za kigeni kwenda nje.

Alieleza kuwa kwa sasa ili kuchochea uzalishaji wa ndani, wanatarajia kuboresha riba kwa wazalishaji wa ndani kutoka asilimia 15 hadi asilimia 25 kwa dawa zote zitakazonunuliwa ndani ya nchi.

Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu alisema kwa sasa wananunua dawa na vifaa tiba kutoka kwa wazalishaji 151 duniani, wazalishaji wa ndani wakiwa ni 18 pekee.

Bwanakunu alisema kwa sasa ni wakati sahihi kwa watu wenye uwezo nchini kuwekeza katika sekta ya uzalishaji wa dawa, kwa kuwa tayari wameshaandaa maeneo matatu muhimu kwa uwekezaji huo.

Alisema uwekezaji wa bidhaa za pamba unatarajiwa kufanyika mkoani Mwanza, bidhaa za maji-tiba mkoani Mbeya na bidhaa za dawa mseto mkoani Pwani.

“Hii ni fursa ya pekee na adimu kwa Watanzania kuwekeza katika maeneo hayo matatu. Kwa hiyo tunachofanya kwa sasa ni kuwahamasisha kujitokeza kwa uwekezaji huo,” alisema.

Mkurugenzi wa Fedha na Mipango wa MSD, Sako Mwakalobo alisema uamuzi huo wa kuweka maeneo ya uwekezaji umekuja ili kupunguza ununuzi wa dawa nje, ambao kwa sasa unafikia zaidi ya asilimia 85 ya dawa zinazonunuliwa na MSD.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles