Nora Damian
Serikali imesema kwa mwaka 2019/20 nchi itakuwa na kiwango cha utoshelevu wa chakula kwa asilimia 119 huku mikoa 11 ikiwa na kiwango cha ziada.
Hali hiyo imebainika baada ya Wizara ya Kilimo kufanya tathmini ya hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula kwa msimu wa 2018/19 na upatikanaji wa chakula kwa mwaka 2019/20 katika mikoa 26 ya Tanzania Bara.
Akizungumza leo Julai 20, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, amesema uzalishaji wa mazao ya chakula kitaifa kwa msimu wa 2018/19, utafikia tani 16,408,309 ambapo nafaka ni tani 9,007,909 na mazao yasiyo ya nafaka ni tani 7,400,400.
Hata hivyo amesema msimu wa uzalishaji wa 2018/2019 ulikabiliwa na changamoto mbalimbali katika baadhi ya maeneo zilizoahiri uzalishaji wa mazao kwa viwango tofauti.
“Katika maeneo yanayopata mvua misimu miwili mvua za vuli katika maeneo mengi hazikufanya vizuri. Mvua za masika pia zilichelewa kuanza na hivyo kuathiri shughuli za kilimo katika maeneo hayo,” amesema Hasunga.