27.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Msekwa: Tumepokea barua ya Makamba, Kinana

Elizabeth Hombo -Dar es salaam

KATIBU wa Baraza la Ushauri la Viongozi Wakuu Wastaafu wa CCM, Pius Msekwa, amesema wanasubiri vikao vya chama hicho tawala kuamua juu ya kile kilichoandikwa katika barua ya malalamiko ya makatibu wakuu wawili wastaafu, kwamba wamedhalilishwa kwa mambo ya uzushi na uongo.

Juzi, makatibu wakuu hao wawili wastaafu wa CCM, Yusuf Makamba na Abdulrahman Kinana, walimwandikia barua Msekwa wakilalamika kudhalilishwa kwa mambo ya uongo na mtu anayejitambulisha kama mwanaharakati na mtetezi wa Serikali.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Msekwa alisema tayari barua ya malalamiko ya wastaafu hao imewafikia na kwamba nyingine kama hiyo pia ilifikishwa kwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. John Magufuli na Katibu Mkuu, Dk. Bashiru Ally.

Msekwa ambaye alisema barua hiyo ambayo ni ya kwanza kuwafikia wao kama Baraza la Wazee Wastaafu, kwa kawaida itapelekwa kwenye chama hicho ambacho ndicho kinachopaswa kuitisha vikao kushughulikia malalamiko yaliyotajwa.

“Hii ni mara ya kwanza kupokea malalamiko ya aina hii, kwanza hakuna utaratibu wa kawaida, lakini tutafuata taratibu za chama, tutapeleka kwenye chama chenyewe.

“Barua hii nakala yake imeenda pia kwa Mwenyekiti wa chama na Katibu Mkuu. Hivyo sisi kama Baraza la Wazee tunasubiri utaratibu wa chama kwanza,” alisema Msekwa.

Alipoulizwa kwanini wakiwa kama Baraza la Wazee hawajakemea mambo hayo kabla hata hawajapelekewa barua, Msekwa alisema kwa mujibu wa Katiba ya CCM kazi yao ni kutoa ushauri.

Katika hilo, Msekwa ambaye amepata pia kuwa Spika wa Bunge, alisema ushauri hautolewi kama amri bali unaombwa.

Jana gazeti hili lilimtafuta Dk. Bashiru mara kadhaa kupitia simu ya mkononi, lakini hakupokea wala kujibu ujumbe mfupi wa maneno aliotumiwa.

Akihojiwa jana na kipindi cha ‘Power Breakfast’ kinachorushwa na kituo cha redio cha Clouds FM, kuhusu ufafanuzi wa barua hiyo, Makamba alimtaka mtangazaji alisome tamko lao kwa sababu linajitosheleza.

“Soma hilo tamko linajitosheleza soma. Je, unalo? Hili tamko halifai kuondolewa koma wala nukta, linatakiwa libaki kama lilivyo, ni tamko refu, ni zuri, tumeliandika vizuri, tumeliandika mimi na rafiki yangu Kinana, halitakiwi kuongezwa kitu, libaki kama lilivyo,” alisema.

Alipoulizwa tamko hilo lina maana gani, Makamba alimwambia mtangazaji; “Wala usiulize, utakapolisoma utalielewa, mbona una haraka? Tafuta, usiwe na haraka.”

Baada ya majibishano hayo, mtangazaji huyo alimwuliza Makamba kama huwa wanaonana mara kwa mara na Kinana na alijibu; “Usitake tena maneno ya umbea kutoka kwangu soma tamko.”

Makamba na Kinana waliopata kushika nafasi ya ukatibu mkuu wa CCM kwa kufuatana wakati wa Serikali ya awamu ya nne, walitoa taarifa ya maandishi kwa umma juzi, huku wakiweka bayana kwamba wamezingatia Katiba ya CCM toleo la mwaka 2017 ibara ya 122.

“Tumewasilisha maombi yetu tukiwasihi wazee wetu watumie busara zao katika kushughulikia jambo hili ambalo linaelekea kuhatarisha umoja, mshikamano na utulivu ndani na nje ya chama.

“Mara kadhaa ametutuhumu sisi wawili, makatibu wakuu wastaafu wa CCM kwa mambo ya uzushi na uongo,” walisema katika barua hiyo.

Vilevile walisema wametafakari kwa kina kabla ya kutoa taarifa kuhusu taarifa wanazodai za uzushi kwa nyakati mbili tofauti.

Walisema kwa sasa Watanzania wanajua kuwa yanayosemwa na mtu huyo si ya kwake.

Kwamba mara kwa mara Watanzania wamekuwa wakijiuliza kwamba mtu huyo (wamemtaja, lakini jina lake tunalihifadhi kwa sababu za kitaaluma) anatumwa na nani.

“Pili anakingiwa kifua na nani? Tatu anatumika kwa malengo gani? Na nne nini hatima ya mikakati yote hii.

“Tafakari yetu inatupeleka kupata majibu yafuatayo; kwanza kwa ushahidi wa kimazingira mtu huyu anatumwa na kutumiwa na watu wenye uwezo wa kumlinda na kumkingia kifua bila kuhojiwa na taasisi yoyote wala mtu yeyote.

“Pili zipo ishara kwamba watu hawa wanaomkingia kifua wana mamlaka, baraka na kinga ambazo wamepewa ili kutekeleza majukumu maalumu kwa watu maalumu na kwa malengo maovu,” walisema katika barua hiyo.

Katika hoja yao ya tatu, walisema mtu huyo anatumika kwa malengo ya kuwazushia, kuwakejeli, kuwavunjia heshima, kuwatia hofu na kuwanyamazisha viongozi, taasisi na watu ambao ni walengwa waliokusudiwa.

“Nne, kuna kila dalili kuwa lengo na hatima ya mkakati huu ni kuandaa tufani ya kuwahusisha walengwa, wastaafu na walio kazini katika nafasi mbalimbali na matendo ya kihalifu, kimaadili na kihaini ili kuhalalisha hayo wanayokusudia kuyafanya.

“Tumeamua kutochukua hatua za kisheria kwa sasa kwa sababu kwanza jambo hili lina taswira ya kimkakati na lina mtandao wenye malengo ya kisiasa. Kwa hiyo linapaswa kushughulikiwa kisiasa.

“Pili, unapochafuliwa, unachokwenda kudai mahakamani ni fidia. Kwetu sisi, heshima yetu haiwezi kuthaminishwa na fidia,” walisema.

Wakizungumzia kuhusu chanzo cha tuhuma hizo, wazee hao walisema wanaamini kuna sehemu zinatoka.

“Yeye anatumwa kutekeleza maagizo na kutumika kama kipaza sauti tu. Huyu ni mamluki anayetumika kuivuruga CCM na nchi yetu. Katika mazingira hayo, hatuwezi kukaa kimya.

“Baada ya kupata ushauri kutoka kwa watu mbalimbali, wakiwemo viongozi wakuu wastaafu wa CCM, viongozi wa dini, wanataaluma, wanahabari, wana-CCM na wananchi kadhaa, tumeamua kutoa tamko kuhusu uzushi anaojitahidi kuueneza,” walisema katika taarifa hiyo.

Aidha walisema mara ya kwanza walizushiwa kwamba wanamkwamisha Rais John Magufuli kutekeleza majukumu yake.

“Tuliyapuuza haya, kwanza kwa imani kwamba viongozi wetu watayaona kwa namna yalivyo kuwa haiwezekani tushiriki kuihujumu Serikali ya chama tulichokitumikia maisha yetu yote.

“Haiingii akilini kwamba wastaafu wawili walio majumbani mwao, wana uwezo wa kumzuia Rais, Amiri Jeshi Mkuu na mwenyekiti wa chama kutekeleza majukumu yake,” ilisema taarifa hiyo.

Walisema kwa mara ya pili wamezushiwa tuhuma nyingine kwamba wanataka kumhujumu Rais ili asipitishwe na CCM kutetea urais mwaka 2020.

“Katika utumishi wetu, tumesimamia michakato ya kupitisha wagombea wa nafasi ya urais na nyinginezo na kwamba tuhuma hizo ni uzushi uliosukwa kwa malengo maalumu na kwamba msingi wa tuhuma zote mbili ni hofu.

“Tuliamini kabisa kwamba pale anapojitokeza mtu hadharani na kuwadhalilisha viongozi waandamizi wastaafu na huku mtu huyo akijinasibisha na Serikali pamoja na Rais ambaye ni mwenyekiti wa CCM, basi hatua zitachukuliwa na taarifa kutolewa kwa umma,” inasomeka taarifa hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles