24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 20, 2024

Contact us: [email protected]

Polisi 54 wafukuzwa kazi, JPM ampa rungu IGP

Nora Damian -Dar es salaam

JESHI la Polisi limewafukuza kazi maofisa, wakaguzi na askari 54 kutokana na utovu wa nidhamu kazini.

Askari hao ni kati ya 157 waliochukuliwa hatua za kinidhamu kuanzia Januari hadi Juni, mwaka huu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa nyumba 20 za makazi ya askari wa Jeshi la Polisi eneo la Magogo mkoani Geita jana, Rais Dk. John Magufuli alilitaka jeshi hilo kuendelea kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya askari wasio waadilifu. 

“Nakupongeza IGP (Simon Sirro) kwa kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya askari 157 ambapo kati yao 54 wamefukuzwa kazi. 

“Ukitaka kazi iende vizuri kufukuza napo kupo ili kama wapo watu wanaenda tofauti, ni wajibu wao kuondoka. Endelea kuwa mkali ili kuimarisha nidhamu kwenye jeshi,” alisema Rais Magufuli.

Alisema askari wengi wanafanya kazi nzuri, lakini wachache wamekuwa wakichafua sifa ya jeshi hilo kwa kuwabambikizia watu kesi, kuhusika kwenye ujambazi na kuonea raia.

“Wengi wanafanya kazi nzuri, mnaofanya kazi vizuri msikatishwe tamaa na askari wachache wanaofanya tofauti na maadili ya kiaskari, endeleeni kusimamia nidhamu katika Jeshi la Polisi,” alisema.

Kuhusu nyumba hizo, alilipongeza jeshi hilo kwa kuzijenga kwa utaratibu wa nguvu kazi na kulitaka kuongeza kasi ya ujenzi wa nyumba nyingine 286, kwani tayari fedha zipo.

Rais Magufuli alipendekeza kambi hiyo iitwe Sirro Barracks ili mkuu huyo wa polisi asimamie nyumba hizo ziishe haraka.

“Usinichomekee mimi, nitashangaa baada ya miaka kadhaa nipite hapa nikute nyumba 20 tu wakati barracks imebeba jina la Sirro. Zikishindwa kukamilika iwe aibu kwako,” alisema.

Pia alilitaka jeshi hilo kuendelea kujipanga kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, unaotarajiwa kufanyika mwaka huu na Uchaguzi Mkuu mwakani.

“Wananchi chagueni viongozi waadilifu, watumishi wa wananchi watakaoweza kutekeleza yale tunayotaka yatekelezwe. Wakiwaletea fedha zao mzile, halafu msiwape kura, chagueni waadilifu watakaowatendea kazi ninyi,” alisema.

Rais Magufuli pia aliahidi kutoa Sh bilioni 1.5 kwa ujenzi wa hospitali ya wilaya katika eneo la Katoro-Buselesele ili kuimarisha huduma za afya.

Ahadi hiyo ilitokana na ombi la Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Msukuma (CCM), aliyesema eneo hilo limekua na kuomba kutanuliwa kwa huduma za afya.

Kuhusu ombi la mbunge huyo la kupelekwa askari wa kike eneo hilo, alimtaka kwanza ajenge nyumba za askari na zitakapokamilika IGP awapeleke.

“Mmeiva (askari) katika mambo yote, inawezekana ndiyo sababu mheshimiwa Mbunge Msukuma anaomba askari wa kike waende huko, sasa IGP usimnyime, mchagulie wanaofanya mazoezi kama haya ya kuzunguka uwapeleke huko, ila tumpe masharti akatengeneze nyumba za askari huko.

“Wanapiga nyimbo nzuri sana, sauti zao nzuri, hata viuno wanajua kukatika vizuri sana, nilifikiri mmekodisha, nikawa nakuuliza IGP na huyo naye ni askari mbona kiuno kinazunguka vizuri. Hongereni sana mazoezi yote mnayajua, mmeiva kisawasawa,” alisema Rais Magufuli. 

Aliwataka wakazi wa mkoa huo kuendelea kuchapa kazi ili takwimu nyingine za uchumi zitakapotolewa usishike mkia kwani una rasilimali nyingi.

“Mkoa huu una madini mengi ya dhahabu, tulipofanya kikao na wafanyabiashara wa madini walieleza changamoto wanazopata, tukafuta baadhi ya kodi na ushuru na tumeanzisha masoko ya dhahabu, muyatumie kuuza dhahabu, msiuze kwenye masoko yaliyofichika ya gizani, msiwauzie dhahabu walanguzi,” alisema.

IGP SIRRO

Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro, alisema matukio ya uhalifu nchini yamepungua kwa kipindi cha Januari hadi Juni mwaka huu, kulinganisha na mwaka jana kipindi kama hicho.

Alisema uhalifu wa jumla umepungua kwa asilimia 2.2, makosa ya barabarani yamepungua kwa matukio 610, ajali zimepungua kwa matukio 175, ajali zilizosababisha vifo zimepungua kwa asilimia 25.7 na waliojeruhiwa wamepungua kwa asilimia 30.8.

Kuhusu tukio la nchini Msumbiji, IGP Sirro alisema hadi sasa watuhumiwa watano wamekamatwa, huku mmoja akitangulia mbele ya haki na kwamba operesheni za pamoja kati ya Msumbiji na Tanzania zinafanyika kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama.

NYUMBA ZA POLISI

Ujenzi wa nyumba hizo za polisi, unatokana na ahadi aliyoitoa Rais Magufuli jijini Arusha mwaka jana ambako alitoa Sh bilioni 10 kujenga nyumba 400 nchi nzima.

IGP Sirro alisema katika awamu ya kwanza, Aprili 2018 walipewa Sh bilioni 3.7 ambapo nyumba 148 zilijengwa na awamu ya pili, Desemba mwaka huo huo, walipewa Sh bilioni 6.3 ambapo nyumba 258 zimejengwa.

Alisema nyumba hizo zimejengwa kila mkoa kutokana na mgawo waliotoa na nyumba moja yenye vyumba viwili vya kulala, sebule, choo, bafu, jiko na mabaraza mawili imegharimu Sh milioni 25.

“Hadi sasa nyumba 114 zimekamilika na zipo tayari kwa matumizi ya askari, nyumba hizi tutazitunza na kufuatilia kwa karibu matumizi yake,” alisema IGP Sirro. 

Pia alimshukuru Rais Magufuli kwa kuwapatia Sh bilioni 3.5 kuwezesha ununuzi wa helkopta mpya, kwani iliyopo ilinunuliwa mwaka 1975.

Alisema chuo cha maofisa wa polisi kilichopo Barabara ya Kilwa, Dar es Salaam kilikuwa hakijakarabatiwa kwa muda mrefu, na kwamba Sh milioni 700 zimewezesha kujenga ghorofa mbili ambazo zinatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu.

“Sh bilioni 123.3 ulizotupatia kulipa malimbikizo ya askari na wazabuni, zimesaidia kwa sababu muda mrefu askari walikuwa hawajalipwa madeni na malimbikizo yao,” alisema.

IGP Sirro alisema wamepatiwa Sh bilioni 5 kununua vifaa vya operesheni na Sh bilioni 10 kulipia nguo za jeshi, huku akionya askari atakayetembea bila sare atashughulikiwa kwa sababu vitambaa na viatu vipo.

Kuhusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, alisema wamejipanga vizuri na hawatamvumilia mtu au kikundi chochote kitakachotaka kuvuruga amani ya nchi. 

“Huwezi kuchagua kiongozi mzuri wakati wa fujo, bali utachagua kiongozi mzuri wakati wa amani, hivyo amani itatamalaki na uchaguzi utapita salama,” alisema.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, alisema nyumba hizo zitakapokamilika, zitapunguza tatizo sugu la upungufu wa makazi ya askari nchini.

“Ili askari waweze kupatikana kwa urahisi wakati wa dharura na kuwadhibiti kinidhamu, wanapaswa kuishi kambini.

“Nakuomba rais uendelee kutusaidia kulingana na mahitaji,” alisema Lugola.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles