MADRID, HISPANIA
KLABU ya Atletico Madrid imeliomba Shikisho la Soka Duniani (FIFA) kuingilia kati kutatua mgogoro wa kipengele cha mkataba, kilichomruhusu Antoine Griezmann, kusajiliwa na Barcelona.
Hatua hiyo , imekuja siku chache baada ya Griezmann kukamilisha uhamisho wake wa kujiunga na Barcelona kwa dau la Euro milioni108.
Mfaransa huyo alianza kuonyesha nia ya kujiunga na mabingwa hao wa Hispania kuanzia msimu uliopita, lakini Wakatalunya hao walisubiri kipengele chake cha mkataba kupungua kutoka Euro milioni 180 hadi 108.
Griezmann anaondoka Atletico, akifunga mabao 133, katika michezo 257 aliyoichezea timu kwa misimu mitano.
Atletico wanadai kuwa, wanalazimika kukubali ofa ya Euro milioni 108, huku wakipanga kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Barca na mchezaji, baada ya kudai makubaliano yalikuwa katika msimu uliopita.
Timu hiyo inafikiria kutinga FIFA , inayohusika ili kukabiliana na mgogoro na kupata haki yao kulingana na thamani ya mchezaji huyo.
Klabu hiyo imeandika “Atletico Madrid inaamini kuwa kiasi cha Euro milioni 108 hakitoshi kufikia kifungu kinachomruhusu kununua mkataba ili kumruhusu kuondoka, kwa kuwa ni dhahiri , ahadi ya mchezaji na Barcelona iliwekwa kabla ya kifungu kilichotajwa hapo, kilipungua kutoka Euro milioni 180 hadi 108.
“Atletico Madrid inaamini makubaliano ya kukomesha mkataba yalifanyika kabla ya mwisho mwa msimu uliopita kutokana na matukio, vitendo na maandamano yaliyofanywa na mchezaji na ndiyo sababu tumeanza taratibu zilizozingatiwa kustahili kulinda haki zetu na maslahi ya halali.