Anna Potinus – Dar es salaam
Rais John Magufuli amemtaka Waziri wa Maliasili na Utalii Khamis Kigwangala, kutenga siku moja ya sherehe ya mavuno ambayo wafanyakazi wa wizara hiyo watajumuika kwa pamoja na kula nyama ili kuwapa motisha ya kuendelea kufanya kazi kwa bidii.
Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo Jumanne Julai 9, wilayani Chato mkoani Geita katika uzinduzi wa Hifadhi ya Taifa ya Burigi – Chato mbapo amesema kuwa si vema wafanyakazi hao kuwalinda na kuwatunza wanyama bila kuruhisiwa kuwala na kwamba iwapo kuna sheria zinapaswa zirekebishwe.
“Nimesekia mmepewa mbogo watano lakini hii yama ni za leo tu isije ikawa mazoe tunataka hawa wanyama tuwatunze wawe wengi lakini Wizara inafahamu vijana hawa na watumishi wa wizara wanafanya kazi nzuri lakini inawezekana hawafaidi sana,” amesema.
“Ukienda Kenya kuna hoteli moja wanauza wanyama pori ni kibali kimetolewa sasa kwanini Waziri usiangalie hata katika kipindi cha miezi mitatu mkapanga angalau siku moja ya sherehe ya kula mazao yenu, nyinyi hamjawahi kuwa na siku ya mavuno kila siku mnawavunia wengine,” amesema
“Ni lazima tujiwekee mikakati hata siku moja angalau hawa vijana wale mnyama haiwezekani kila siku wanawatunza tu hawa wanyama halafu hawaruhusiwi kuwala hivyo kama kuna sheria za kubadilisha badilisheni, huu ni ufugaji mbaya, ni lazima mtengeneze mazingira mazuri yatakayokuwa yanawapa wafanyakazi wa Wizara yenu kuwa na motisha ya kufanya kazi,” amesema.