Safina Sarwatt – Hai
Serikali imeanza utekelezaji wa kufufua kiwanda cha kutengeneza vipuli vya viwandani na magari cha Mashine tools kilichopo wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, ambacho kilisimamisha uzalishaji kwa zaidi ya mika 30.
Waziri wa viwanda na biashara Innocent Bashunga amethibitisha jambo hilo leo Alhamisi Julai 4, wakati wa akizindua matengenezo ya tela za trekta mpya katika kiwanda hicho ambapo amezitaka taasisi zinazotengeneza zana za viwandani kuzalisha bidhaa bora zitakazowasaidia wakulima wadogo ili kufikia malengo ya serikali ya uchumi wa viwanda.
Amesema kuwa tayari serikali imeridhia ombi la Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro la kufufua viwanda ambavyo vimekufa kwa muda mrefu na kwamba lazima mkakati huo uende sambamba na kubadilisha maisha ya wakulima wadogo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Anna Mghwira, amesema mpango wa kufufua kiwanda hicho kitakuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi mkoani humo na kwamba kuna wawekezaji kutoka nje ambao wameonyesha nia ya kuja kuwekeza katika kiwanda hicho.