Asha Bani, Dar es Salaam
Serikali imeagiza wabunifu mbalimbali nchini kufuatwa maeneo ya vijijini ili waweze kuonesha kazi zao kutumika na kuleta manufaa kwa taifa.
Hayo yameelezwa leo Jumatano Julai 2, na Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu, Sayansi Teknolojia na Ufundi, William Ole Nasha alipokuwa katika banda la maonesho la Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ambapo amewataka kuongeza nguvu ya kuwafuata wabunifu waliopo maeneo ya vijijini na kuwasaidia kuonekana kwa kazi zao.
“Nimetembelea mabanda takribani nane yaliyokuwa chini ya wizara hii lakini nimeona kuna wabunifu wengi wapo na wanabuni kazi mbalimbali zenye uwezo mkubwa wa kusaidia taifa hili hivyo ni vyema wakafuatwa katika maeneo yao na Costech mkawa katika mstari wa mbele kuwasaidia wabunifu hao.
“Mfano nikiwa katika banda la Mamlaka ya Elimu na Ufundi Stadi (VETA) nimeona wabunifu wa mitambo ya umeme unaosaidia katika masuala mbalimbali ya kiusalama hii itasaidia mkaweza hata kuwapa mitaji wakafanya vizuri zaidi kwa kushirikiana na mashirika makubwa kama Shirika la Umeme nchini (Tanesco),” amesema.
Katika banda la VETA kuna mbunifu amefanikiwa kutengeneza mfumo unaopiga simu wenye kama eneo la nyumba lina hatari ikiwamo gari au lifti.