Bethsheba Wambura, Dar es Salaam
Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa amesema wizara yake kwa kushirikiana na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), wataanza kwenda kila wilaya na mkoa ili kukutana ana kwa ana na wafanyabishara kujua changamoto wanazokutana nazo hatimaye kuzitatua.
Amesema amefikia hatua hiyo baada ya Rais John Magufuli kufanya kikao na wafanyabiashara Juni 17, Ikulu jijini Dar es Salaam ambapo kila wilaya iliwakilishwa na wafanyabiashara watano kikao ambacho kiliwawezesha kuzisema changamoto zao na zikatatuliwa na zinaendelea kutatuliwa.
Akizungumza leo Jumanne Julai 2, wakati wa uzinduzi wa Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) ya 43, uliofanyika katika viwanja vya sabasaba jijini Dar es salaam, Bashungwa amesema kwa kufanya hivyo wataongeza ufanisi katika biashara hapa nchini.
“Rais Magufuli amenionyesha njia namna wizara yangu inapaswa kuwa karibu na wafanyabiashara wadogo na wa kati, tutaenda kila wilaya kutatua changamoto wanazokumbana nazo wafanyabiashara mikoani,” amesema Bashungwa.
Aidha Bashungwa ametoa rai kwa kila halmashauri nchini kutenga maeneo ya viwanda ili iwe rahisi kwa wawekezaji kupata maeneo ya uwekezaji.