Membe awataka viongozi wa dini, wastaafu kukemea utekaji, azungumzia Lissu kuvuliwa ubunge

0
1228

Kulwa Mzee, Dar es Salaam

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe amewataka viongozi wa dini, serikali na wastaafu kukemea suala la utekaji kwani haiwezekani watu kuishi nchini kwa wasiwasi.

Akizungumza na waandishi wa habari katika viunga vya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, leo Jumanne Julai 2, wakati alipokuja kusikiliza kesi ya madai aliyofungua dhidi ya mmiliki wa gazeti la Tanzanite, Cyprian Musiba na wachapishaji wa gazeti hilo.

“Kama Mtanzania ninashangaa, huu utekaji au kupotea watu kunaweza kuondoa amani na usalama wa nchi.

“Nawaomba viongozi walikemee hili lisitokee, tutazuia watalii kuja kama hali hii itaendelea, ni utamaduni ambao hatukuwa nao tangu awali, viongozi wote wastaafu na viongozi wa dini wasilikwepe hili lazima tukemee utamaduni huu mpya,” amesema Membe.

Aidha, akizungumzia kuhusu Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kupoteza ubunge, Membe amesema kama Mtanzania ameshangaa sana.

“Mimi kama Mtanzania  nilishangazwa sana na uamuzi wa Spika, Job Ndugai lakini tusubiri Lissu arudi.

“Nina uhakika atakwenda mahakamani kudai haki yake na kama ipo haki ataipata mahakamani,” amesema Membe

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here