KULWA MZEE-DAR ES SALAAM
DAKTARI wa Hospitali ya Polisi Kilwa Road, Juma Alfani (54), ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jinsi alivyowahudumia askari wawili waliojeruhiwa katika maandamano yaliyofanywa na wafuasi wa Chadema, Februari 16, mwaka jana.
Dk. Alfani ambaye ni shahidi wa tano, alitoa ushahidi jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba akiongozwa na Wakili wa Serikali, Salim Msemo.
Alidai alisajiliwa na Baraza la Madaktari Tanganyika mwaka 2014, akapewa namba 2660 na majukumu yake ni kutoa huduma zote za kitabibu pamoja na upasuaji.
“Katika utendaji wangu wa kazi naongozwa na miiko, ikiwemo kutotoa siri za mgonjwa, isipokuwa pale inapohitajika kufanya hivyo,” alidai.
Alidai Februari 16, mwaka jana saa 5:40 usiku alikuwa daktari wa zamu katika wodi ya wazazi, alifuatwa na nesi akimweleza kwamba katika chumba cha dharura kuna wagonjwa wawili wanaume.
“Mgonjwa mmoja alikuwa anapiga kelele… alikuwa anavuja damu kichwani, akilalamika maumivu makali na mkononi.
“Mgonjwa mwingine alikuwa akiweweseka, alipiga kelele yuko wapi hapa… maumivu, niliwauliza manesi kama wameshapata huduma, wakasema bado, nikawaelekeza wachomwe sindano za kutuliza maumivu, walichomwa wakatulia.
“Koplo Fikiri aliyekuwa anatoka damu kichwani nilipomuhoji alidai walikuwa Mkwajuni wanatuliza maandamano ndio akajeruhiwa, nilielekeza awekewe drip,” alidai.
Alidai alikwenda kumuhudumia Koplo Rahim ambaye shingo yake ilivimba na alikuwa hawezi kugeuka, ambaye alidai akiwa katika maandamano alishtukia kitu kimemgonga.
Shahidi alidai asubuhi alielekeza wagonjwa wafanyiwe vipimo kuona jinsi walivyoumia na Februari 20, mwaka jana aliwaona wagonjwa wakiendelea vizuri.
Washtakiwa katika kesi hiyo ya uchochezi ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu bara na Mbunge wa Kibamba John Mnyika, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya, Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko, Katibu Mkuu, Dk. Vincent Mashinji na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa.
Kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13, yakiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari mosi na 16, mwaka 2018, Dar es Salaam.