MWANDISHI WETU-DAR ES SALAM
WAKATI Serikali ikipambana kuhakikisha kila Mtanzania anayestahili kulipa kodi anafanya hivyo, baadhi ya wamiliki wa nyumba eneo la Kariakoo, Dar es Salaam, imebainika wamekuwa wakikwepa kodi kwa kuwa na mikataba miwili kwa wapangaji wao.
Hatua hiyo inatokana na baadhi ya wenye nyumba hao kupangisha fremu za maduka kwa gharama ya Sh milioni moja kwa mwezi, huku mkataba wa pili ambao huandikiwa kodi ya Sh 200,000 ndio huwasilishwa TRA kwa makadirio ya kodi.
Kitendo hicho kimezua taharuki na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara, ambao wengine sasa wamebaki wakishindwa kujua la kufanya, hasa inapofika kipindi cha malipo ya kodi ya pango, kwamba wanatakiwa kulipa kwa mkataba wa aina gani.
Uchunguzi uliofanywa na MTANZANIA kwa zaidi ya miezi miwili katika eneo la Kariakoo, ulibaini ulaghai mkubwa unaofanywa na baadhi ya wenye nyumba, ambao wamekuwa wakitumia mwanya huo kama njia ya kukwepa kodi ya Serikali jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Moja ya mikataba ambayo gazeti hili linayo nakala yake unaonesha kwamba mwenye nyumba Himdat Mohammed Mzamil, aliingia mkataba wa awali na mpangaji wake Juma Nassor (Si jina lake halisi) wa kulipa kodi ya pango ya Sh 800,000 kwa mwezi, huku mwingine akiuandaa kwa Sh 200,000 kwa mpangaji huyo huyo.
Mbali na hilo, pia mkataba mwengine ulimuhusu mwenye nyumba Ahmed Gullah ambaye alimpangisha fremu ya duka Suzan Joseph (si jina lake halisi) kwa Sh milioni 1.5, huku mkataba mwingine akiuandika wa Sh 500,000 kwa mwezi.
KAULI ZA WAPANGAJI
Mmoja wa wapangaji wa majengo hayo yaliyopo Mtaa wa Kongo, ambaye hakuwa tayari kutajwa jina lake gazetini, alisema suala la kuwa na mikataba miwili imekuwa ni mchezo wa wenye nyumba wengi wa Kariakoo.
Alisema pamoja na hali hiyo, tayari wamekuwa wakilalamikia suala hilo jambo ambalo bado wanakosa la kufanya kwani wana hofu kama wakiendelea na ukaidi huenda wakajikuta kwenye hatari wa kufukuzwa na wenye nyumba.
“Ni kweli hata mkataba wangu (anaonesha) uko hivi, kodi halali ninayotakiwa kulipa ni Sh milioni moja, lakini nimepewa mkataba wa pili ambao unaonesha Sh 300,000 sasa unafikiri ninafanyaje kwa hali hii.
“Tunajua kwa sasa Serikali kupitia Rais Magufuli (Dk. John Magufuli), imekuwa na kazi kubwa ya kuhakikisha inawashughulikia wakwepa kodi, lakini tunapenda wafanye ukaguzi maalumu kama mlivyokuja nyie waje waone.
“Wanachukua mikataba ambayo tumeandikiwa bei ndogo ndiyo wanapeleka TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania), ambayo huonyesha na kwenye kukadiriwa kodi hulipa kidogo wakati kwetu huchukua fedha nyingi,” alisema mfanyabiashara huyo.
Naye Said Juma, alisema kuwa kitendo cha kuwa na mikataba miwili katika majengo yao kinazua vurugu kwani wakati mwingine mpangaji hujikuta akihamishwa kwa nguvu na mwenye nyumba pindi anapohoji alipe kodi ya mkataba upi.
“Hivi karibuni hapa kwenye jengo la jirani yetu yupo dada mmoja ambaye alikuwa mfanyabiashara mkubwa sana wa madera, naye alijikuta kwenye mgogoro mkubwa na mwenye nyumba wake, yule dada alikuwa na mkataba wa kwanza wa Sh 800,000 na wa pili wa Sh 200,000. Wamesumbuana na mwenye nyumba mwisho ametumia nguvu kumuhamisha.
“Ninayasema haya ili tu muone hali halisi ilivyo hapa Kariakoo, kwa kweli hali inatisha sana. Serikali ikiwa pembeni inahisi sisi tunafanya biashara sana ila hawajui machungu tunayopitia sisi, kifupi Kariakoo ina wakwepakodi wengi ambao si wafanyabiashara, bali ni wenye nyumba,” alisema Juma.
KAULI YA MWENYE NYUMBA
Mmoja wa wenye nyumba ambao wanatajwa kuwa katika mchezo huo mchafu wa kuandaa mikataba miwili kwa wapangaji, Yussuf Mzamil, ambaye anasimamia jengo la Himdat Mohammed Mzamil, alisema suala la kuwa na mikataba miwili yeye hausiki nalo ila wakati mwingine hufanya hivyo kwa kuombwa na wapangaji wenyewe.
“Ninashindwa la kusema katika hili, ila kwa kifupi ni kwamba ni kweli ipo mikataba miwili ambayo hutolewa, lakini wakati mwingine huwa ninaombwa na wapangaji ili waweze kukopa benki,” alisema Yussuf.
Alipoulizwa kama huombwa na wapangaji, ni mkataba upi ambao wao huwasilisha TRA kwa makadirio ya kodi, alishindwa kueleza zaidi ya kuomba muda ili aweze kujibu kwa kina madai hayo.
“Wakati mwingine wema wangu huniponza… nipe muda nitajibu,” alisema.
Na zilipopita zaidi ya wiki mbili, alipotafutwa tena, alijibu kwa kifupi; “Naona mmeamua mnataka kunichongea kwa Serikali, sawa, sina la kusema mimi jamani,” alisema na kukata simu.
KATIBU WA WAFANYABIASHARA
Katibu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania, Abdallah Mwinyi, alisema wanajua suala hilo, lakini hawezi kuliongelea sana kwa kuwa yeye mwenyewe ni mfanyabiashara, hivyo atakuwa anajiweka katika hali ya hatari hata na mwenye nyumba wake.
“Hayo yote wameyataka Serikali wenyewe, sisi tulilalamika hata kwa maandishi kuna vitu ambavyo vinatakiwa kufanyiwa marekebisho, hata hivyo siwezi nikaongea sana nikasababisha kujitenganisha na wafanyabiashara wenzangu, nisije kufukuzwa bure kwa kuwa hapa nilipo pia nimepanga,’’ alisema Mwinyi.
KAULI YA TRA
Akizungumzia hali hiyo, Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi kutoka TRA, Richard Kayombo, alisema wana taarifa za hujuma hiyo na wameanza kufanyia kazi kwa kuelekeza timu yao kufanya msako na kuchukua hatua.
“Lakini pia tumekuwa na utaratibu kwa sasa wa kukagua maeneo hayo ya biashara na kutathmini na kuweka sisi wenyewe kiwango cha kodi pasipo kuangalia mikataba hiyo ambayo ni ya udanganyifu,’’ alisema Kayombo.
MSIMAMO WA JPM
Juni 7, mwaka huu wakati akizungumza a wafanyabiashara zaidi ya 1,000 Ikulu Dar es Salaam, Rais Dk. John Magufuli, alisema rushwa zinazotozwa na maofisa wa Serikali na udanganyifu unaofanywa na wafanyabiashara, ni baadhi ya vikwazo vikubwa vinavyoandama ukuaji wa biashara na uchumi nchini.
Alisema japo kuna jitihada kubwa zinazofanyika kupambana na rushwa, bado kuna maofisa wa Serikali si waaminifu, na aliyataja maeneo yanayoongoza kwa rushwa ni bandarini, TRA, barabarani na mipakani.