24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Mbunge wa Kenya aliyetaka Watanzania wapigwe akamatwa

NAIROBI – KENYA

MBUNGE wa Kenya, Charles Kanyi maarufu kama Jaguar, aliyetoa saa 24 kwa wafanyabiashara wa Tanzania na Uganda kuondoka nchini humo, vinginevyo watawaondoa kwa nguvu na kwa kipigo, amekamatwa.   

Jaguar ambaye pia ni mwanamuziki, alikamatwa jana mchana na maofisa wa Jeshi la Polisi nchini Kenya akiwa katika viwanja vya Bunge.

Ingawa sababu za kukamatwa kwake hazijawekwa wazi, lakini tukio hilo linaunganishwa na kauli yake ya chuki dhidi ya wafanyabiashara kutoka nchi nyingine, zikiwamo  Tanzania na Uganda, wanaoendesha shughuli zao jijini Nairobi ambao alisema wamechukua nafasi ya Wakenya.

Kauli yake hiyo ambayo mbali na kusambaa katika mitandao ya kijamii na kuzua mjadala mkubwa, iliilazimisha Serikali ya Tanzania kupitia kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kulieleza Bunge kuwa imechukua hatua ya kumwita balozi wa Kenya kujieleza.

Majaliwa alisema waliichukua kauli hiyo kwa umuhimu mkubwa na balozi wa Kenya alisema lilikuwa tamshi binafsi ambalo halihusiani na msimamo wa Serikali.

Alisema balozi huyo aliahidi kwamba Serikali ya Kenya  itamuhoji mbunge huyo kuelezea kile alichomaanisha katika matamshi yake.

“Watanzania wataendelea kuwa salama nchini Kenya,” Majaliwa aliliambia Bunge ambalo lilitaka kufahamu msimamo wa Serikali juu ya kauli ya mbunge huyo ambayo ilileta sintofahamu kwa raia wa mataifa aliyoyataja.

Zaidi Serikali ya Kenya nayo ililazimika kutoa taarifa kueleza msimamo wake, kwanza ikipinga kauli hiyo, lakini pili ikieleza kuwa katika mazingira ya sasa ya utandawazi haina nafasi.

Serikali ya Kenya katika taarifa yake hiyo ilieleza kuwa katika mazingira ya wastaarabu, wao kama taifa wanaoishi kwa amani na kupenda wageni wa mataifa mbalimbali, matamshi hayo hayana nafasi.

Katika hilo, Serikali ya Kenya ilisema watu wote wenye matamanio ya kuwekeza nchini humo usalama wao ni jambo wanalolipa kipaumbele.  

Katika video fupi inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii, mbunge huyo anasikika akisema hawatokubali raia wa nje waende kuendesha biashara nchini Kenya.

“Mimi naipa Serikali saa 24, kama hao watu hawatakuwa wamerudi kwao, tutaingia kwa hayo maduka wanayofanyia kazi na kuwatoa, tutawapiga na kuwapeleka katika uwanja wa ndege.

“Kwa hivyo mimi naomba waziri waangalie hii maneno, wahakikishe kuwa Wakenya wetu wanafanya biashara bila ya kushindana na wageni kutoka nchi mbalimbali.

“Ukiangalia vile magari yanavyouzwa hapa, Wapakistan wamechukua hiyo biashara, ukiangalia nyamakima Wachanise wamechukua hizo biashara, ukiangalia masoko zetu, Watanzania na Waganda wamechukua hizo biashara.

“Wakenya ni sharti wafanye biashara zao bila kushindana na watu kutoka mataifa mengine… Tunasema imetosha, iwapo hawatarajeshwa nyumbani katika saa 24 tutawashika na kuwapiga na hatuogopi mtu yeyote,” anasikika mbunge huyo.

Pamoja na Kenya kutoa msimamo wake wa kujitenga na  matamshi ya mbunge huyo, mijadala katika mitandao ya kijamii bado imeendelea kuwa mikali, huku baadhi wakimtaka mbunge huyo aombe radhi.

Kupitia akaunti ya mtandao wa Twitter, inayosadikika kumilikiwa na mbunge huyo, aliandika; “Kile nilichokisema hivi karibuni juu ya wageni kuvamia katika soko letu kimetafsiriwa vibaya… namaanisha amani kwa nchi yangu, biashara lazima ziendelee pasipo kuingiliwa na wageni, wote mnakaribishwa katika nchi yetu.” 

Soko kubwa la mitumba la jijini Nairobi la Gikomba, ambalo Jaguar alilitumia kutoa kauli hiyo ya kuudhi hivi karibuni, lipo ndani ya Jimbo la Starehe.

Kauli ya mbunge huyo imekuja katika wakati ambao ni wiki iliyopita tu Serikali ya Kenya iliwatimua raia saba wa China kwa kuendesha ujasiriamali katika soko kubwa la Gikomba bila ya kuwa na vibali halali vya kuwa nchini humo.

Waziri wa Usalama wa Kitaifa, Fred Matiangi alikaririwa akisema Serikali ilisitisha kuwapa vibali vya kazi wajasiriamali wote.

Kwamba yeyote anayetaka kibali cha kazi atatuma maombi akiwa nchini mwake, atafika Kenya iwapo atakuwa na kibali hicho.

Alisisitiza kuwa Serikali haiwapi wafanyibiashara vibali vya kazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles