PYONGYANG, KOREA KASKAZINI
KIONGOZI wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un na mwenzake wa China, Xi Jinping, wamekubaliana kuimarisha urafiki wa mataifa hayo mawili bila kujali mwenendo wa siasa za kimataifa.
Shirika la Habari la Korea Kaskazini limeripoti kwamba viongozi hao wawili wamezungumzia mfululizo wa mipango ya kuimarisha ushirikiano ikiwemo masuala ya kisera wakati wa siku ya mwisho ya ziara ya Xi mjini Pyongyang.
Hata hivyo, hakuna maelezo ya ziada yaliyotolewa kuhusu makubaliano yaliyofikiwa.
Rais Xi ameondoka Korea Kaskazini baada ya ziara ya siku mbili ambayo ni ya kwanza kufanywa na kiongozi wa China katika kipindi cha miaka 14 iliyopita.
Ziara ya Rais wa China nchini Korea Kaskazini imelenga kuonesha mshikamano na taifa hilo linalokabiliwa na shinikizo la vikwazo vya Umoja wa Mataifa kutokana na mpango wake tata wa silaha za nyuklia.