Derick Milton-Simiyu
Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini, Kamishina Jenerali Thobias Andengenye, amesema jeshi hilo kwa kushirikiana na serikali wanatafuta mkopo wenye masharti nafuu ili kuweza kununua magari ya kuzima moto na vifaa vingine.
Amesema hayo leo Juni 18, wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Simiyu, ambapo amekiri kuwepo kwa changamoto kubwa ya ukosefu wa magari ya kuzimia moto.
“Jeshi la zima moto kwa kushirikiana na serikali tupo katika mchakato wa kutafuta mkopo wenye masharti nafuu, ambao kama utapatikana tutaweza kununua Magari na vifaa vingine vya kuzimia moto,” amesema.
“Tangu serikali ya awamu ya tano imeingia madarakani imekuwa ikitenga bajeti ya maendeleo kwa jeshi la zimamoto ambayo imekuwa ikitumika kwa ajili ya kununua magari na vifaa vya kupambana na majanga ya moto,” amesema.
Aidha ameongeza kuwa jeshi hilo limeanzisha mpango wa kutoa elimu ya kawaida kupitia nyumba za ibada kwa wananchi juu ya kuwa na uwezo wa kupambana na ajali za moto wa awali kabla ya kuhitaji msaada kutoka jeshi hilo.