LAGOS, NIGERIA
NAHODHA wa timu ya taifa ya Nigeria, John Obi Mikel, ameweka wazi kuwa, michuano hii ya Mataifa ya Afrika nchini Misri, itakuwa ya mwisho kuitumikia timu hiyo.
Mchezaji huyo amekuwa kwenye kikosi cha timu hiyo tangu alipopata nafasi mwaka 2005 katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Libya, lakini sasa anaamini umri wake unazidi kuwa mkubwa na ni wakati wa kuwapisha wachezaji chipukizi.
Kiungo huyo wa zamani wa Chelsea, alitajwa kwenye kikosi cha mwisho cha wachezaji 23 wa kuelekea nchini Misri chini ya kocha wao Gernot Rohr.
Hii itakuwa ni mara yake ya nne kushiriki michuano ya Afcon, mara ya kwanza kushiriki ilikuwa 2006, akashiriki tena mwaka 2008 pamoja na 2013.
“Sijui kama nitakuwepo tena kwenye Afcon mwaka 2021 huko nchini Cameroon, hii inaweza kuwa ni nafasi yangu ya mwisho kucheza Afcon, napenda kwenda kushiriki kila mwaka, lakini vijana wapo wengi sana, hivyo kabla ya Afcon ijayo nitakuwa na miaka 34, ila sina uhakika sana kama nitakuwa na asilimia 100 ya kushiriki,” alisema mchezaji huyo.